| Add caption |
Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya siasa nchini imemuandikia barua Katibu Mkuu wa
Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad kufuatia mvutano wa
kusimamishwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Profesa
Lipumba kumuandikia barua Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji
Francis Mutungi akilalamikia kusimamishwa uanachama bila kufuata
utaratibu huku akitaka kurejeshwa kwenye nafasi yake ya uenyekiti.
Ofisi hiyo imeutaka uongozi wa CUF
kueleza kwa kina hatua ilizopitia hadi kufikia uamuzi huo kwa mujibu wa
katiba ya chama hicho, na kwamba iwasilishe barua hiyo kufikia kesho
majira ya saa 9:30 alasiri.
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano cha
Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa, Monica Laurent amesema kuwa ofisi
hiyo ilipokea barua ya Profesa Lipumba Agosti 29 mwaka huu ikiwa na
malalamiko na kwamba wametaka uongozi wa CUF kutolea majibu.
“Tumeitaka CUF kutoa majibu kuhusu malalamiko ya Profesa Lipumba, ndipo sisi tutakapotoa majibu,” amesema Monica.
Lipumba ambaye alijiuzulu nafasi yake
ya Uenyekiti mwaka jana akipinga uamuzi wa chama chake kumuunga mkono
Edward Lowassa kugombea urais, amerejea na kudai kutengua barua yake ya
kujiuzulu.
Baraza Kuu la CUF lililoketi visiwani
Zanzibar hivi karibuni lilimsimamisha uanachama Profesa Lipumba pamoja
na viongozi wengine 10 akiwemo Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya
aliyekuwa Naibu Katibu mkuu (Bara).
Hata hivyo, Profesa Lipumba amepinga uamuzi huo akieleza kuwa kikao cha baraza hilo kililiwa batili.