Wafanyakazi hao waliangua kilio baada ya
mkuu huyo wa mkoa kufanya ziara ya kushitukiza kukagua barabara kwa
lengo la kuangalia maendeleo yake wiki iliyopita.
Mara baada ya mkuu wa mkoa huyo kufika
eneo la mradi, walimueleza wamekuwa wakitumikishwa bila kuwa na mikataba
ya ajira na wamekuwa wakifanya kazi kwa zaidi ya saa 14 kwa siku bila
kulipwa muda wa ziada, badala yake wanalipwa shilingi 10,000 tu na
wanapodai haki zao, wanafukuzwa kazi.
Mfanyakazi mmoja aliyejitambulisha kwa
jina moja tu la Daniel alisema Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipotembelea mradi huo hivi karibuni,
walimueleza kero hiyo. “Waziri Mbarawa alitoa mwezi mmoja kwa mkandarasi
huyo kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wote 400 lakini mpaka sasa
hakuna utekelezaji uliofanyika,” alilalamika Daniel.
Akijibu tuhuma hizo, Msimamizi wa Mradi
wa Kampuni, Mhandisi Mbaraka Shafii alisema kampuni yao imeshatoa
mikataba kwa baadhi ya wafanyakazi na kwamba mchakato huo bado
unaendelea ili wafanyakazi wote wapate mikataba yao kama Waziri Mbarawa
alivyoagiza.
Akizungumzia kero hiyo, mkuu wa mkoa
huo, Ntibenda alimtaka mkandarasi huyo kutoa mikataba ya kazi kwa
wafanyakazi wote mara moja na aache kuwatumikisha muda wa ziada bila
kuwalipa stahiki zao.
“Pia hakikisheni barabara hii inajengwa
kwa kiwango kinachotakiwa na msipofanya hivyo, kampuni hii itachukuliwa
hatua za kisheria mara moja,” alionya Ntibenda.
Barabara ya Sakina–Tengeru yenye urefu
wa kilomita 14 inajengwa kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na
inatakiwa iwe imekamilika na kukabidhiwa kwa serikali ifikapo Mei
mwakani.