Septemba Mosi, 2015, Sheria ya
Makosa ya Mtandao (The Cybercrimes Act, 2015) ilianza kutumika rasmi
nchini Tanzania, baada ya muswada wake kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuwa sheria lakini uchunguzi wa gazeti hili,
umebaini kwamba bado wengi hawajui namna ya kuitumia sheria hiyo.
Licha ya kupungua kwa kiasi kikubwa kwa
makosa ya mtandao tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo, bado vipo
vitendo vya uvunjaji wa sheria vinavyoendelea kutokea kila kukicha,
ikiwemo watu kutukanwa mitandaoni, kupostiwa kwa picha za utupu,
kutishiwa maisha na kudhalilishwa.
Zikiwa zimesalia siku kadhaa kutimia kwa
mwaka mmoja tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo, gazeti hili
limechimba hatua tano zinazoweza kutumika kumfikisha mhalifu wa makosa
ya mtandao kortini pamoja na mbinu ambazo kila mmoja anapaswa kuzifuata
ili kuwa salama na sheria hii.
HALI ILIVYOKUWA AWALI
Kabla ya kupitishwa kwa sheria hiyo ya
makosa ya mtandao, wimbi la matukio ya watu kudhalilishwa mitandaoni,
ikiwemo kuwatumia meseji za matusi, kuposti picha zao za utupu kwenye
mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na mingineyo, kuibiwa pesa
kwa njia za mtandao wa simu sambamba na kudukua (hacking) akaunti za
watu kwenye mitandao ya kijamii, lilikuwa kubwa na lilifikia hatua ya
kutishia usalama wa wananchi na mali zao.
Hata hivyo, tangu kuanza kutumika kwa
sheria hiyo, makosa hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa ingawa bado
hayajakoma kabisa. Wanaofanyiwa makosa hayo, kama wanajua nini cha
kufanya, sheria imekuwa ikiwasaidia kupata haki zao lakini kama ulikuwa
hujui nini cha kufanya ili kupata haki yako, mwandishi wetu amewasiliana
na Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao wametoa ufafanuzi ufuatao.
TCRA WANASEMAJE?
Wiki iliyopita, mwandishi wetu alifunga
safari mpaka makao makuu ya TCRA na kufanikiwa kuzungumza na Afisa
Mawasiliano Mkuu, Semu Mwakyanjala kuhusu sheria ya makosa ya mtandao na
hatua za kufuata sheria inapovunjwa.
Kabla ya yote, Mwakyanjala alimueleza
mwandishi wetu kwamba sheria hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza
makosa ya kimtandao ingawa bado wapo wanaoendelea kuvunja sheria ambao
nao wanakumbana na dola.
Alipoulizwa ni makosa mangapi mpaka sasa
yamesharipotiwa kwake na namna walivyoyashughulikia, Mwakyanjala
alisema wao hawashughuliki na wahalifu wa kimtandao moja kwa moja badala
yake, huwa wanaletewa taarifa na jeshi la polisi, kitengo cha Cyber
Crime Unit ambao ndiyo wanaoshughulika moja kwa moja na wanaovunja
sheria hiyo.
Mwakyanjala akaongeza kuwa taarifa
zaidi, anaweza kuwa nazo bosi wake, Innocent Mungi ambaye ndiye Meneja
wa Mawasiliano wa TCRA. Akamtaka mwandishi wetu kumtafuta Mungi kupitia
namba ya simu ya mkononi aliyomtajia mwandishi wetu.
HATUA TANO ZA KUFUATA
Mwakyanjala alimueleza mwandishi wetu
kwamba licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, bado watu wanaojitokeza kuomba
msaada wa kisheria ni wachache, akaeleza kuwa huenda Watanzania wengine
ni waoga au hawajui taratibu. Mwandishi wetu alipomuuliza taratibu za
kufuata mtu anapofanyiwa makosa ya kimtandao, Mwakyanjala alitoa
ufafanuzi wa nini cha kufanya.
- HATUA YA KWANZA
Mtu anapofanyiwa makosa ya kimtandao,
iwe ametukanwa, picha yake ya utupu imepostiwa mtandaoni, akaunti yake
imedukuliwa, ameibiwa pesa au vinginevyo, hatua ya kwanza anatakiwa
kwenda polisi kuripoti tukio hilo akiwa na vielelezo vyake.
- HATUA YA PILI
Baada ya kufungua jalada kituo cha
polisi, mshtaki atasaidiana na polisi kuwasiliana na kitengo cha Cyber
Crime Unit kilichopo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi (Wizara ya Mambo ya
Ndani ) ambao nao wataanza kulichunguza kwa kina suala hilo.
- HATUA YA TATU
Baada ya kuchunguza kwa kina, polisi wa
kitengo cha Cyber Crime kama watahitaji ushahidi wa kitaalamu zaidi,
watawasiliana na makao makuu ya TCRA ambao watawapa maelezo yote kwa
kina, kuhusu mtu aliyefanya uhalifu huo, mahali ulipofanyika, muda na
jinsi ulivyofanyika.
Polisi hao wa Cyber Crime Unit, watashirikiana na polisi wa kituo ilipofunguliwa kesi na mhusika mwenyewe.
- HATUA YA NNE
Baada ya vielelezo vyote kukamilika
ikiwa ni pamoja na ushahidi, mtuhumiwa atakamatwa na polisi na
kufunguliwa jalada la mashtaka kulingana na makosa aliyoyafanya.
- HATUA YA TANO
Mtuhumiwa atapandishwa kizimbani na
kusomewa mashtaka yanayomkabili ambapo akikutwa na hatia, atahukumiwa
kulingana na uzito wa kosa alilolifanya ambapo hukumu inaweza kuwa ni
kwenda jela, kulipa faini au vyote kwa pamoja.
POLISI WANASEMAJE?
Itaendelea wiki ijayo