Kauli ya Rais ya Kuzuia Vyama
vya Siasa Kufanya Shughuli za Siasa kwa Miaka Mitano ni Tangazo la Vita
dhidi ya Demokrasia na Mfumo wa Vyama vingi Nchini
Tumepokea kwa MSHTUKO na masikitiko
makubwa kauli ya rais kwamba vyama vya siasa havipaswi kufanya siasa
isipokuwa wakati wa kampeni na kupitia bungeni.
Kimsingi kauli ya rais ni kauli yenye
nia ya kuvunja Sheria ya Vyama vya Siasa inayolinda uwepo wa mfumo wa
vyama vingi na kuhimiza vyama vya siasa kufanya shughuli za siasa katika
msimu wote ili kuthibitisha uhai wao.
Tunaichukulia kauli ya rais kama
tangazo la vita dhidi ya demokrasia na uhai wa vyama vingi nchini. Chama
chetu kitaitisha vikao vya dharura kujadili hali ya siasa nchini na
namna ya kukabiliana na mashambulizi yanayoendelea dhidi ya demokrasia
nchini mwetu.
Tunatoa wito kwa vyama vyote vya siasa
vinavyoamini katika misingi ya demokrasia nchini kukutana haraka na
kujadili namna ya kuunganisha nguvu pamoja katika kupigana vita mpya ya
kulinda demokrasia nchini mwetu.
Aidha, tunatoa wito kwa wananchi wote
na taasisi za kiraia kusimama imara katika kulinda demokrasia.
Tunasisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi duniani kote unaonyesha kuwa
huwezi kuua demokrasia bila kuua juhudi za maendeleo. Tusiruhusu mtu
yeyote mwenye mamlaka kuua demokrasia nchini mwetu.
Hatua zozote za kuua demokrasia ni
kuua Umoja, Amani na Mshikamano wa wananchi na Taifa, ambayo ndiyo
misingi ya maendeleo ya nchi yetu kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Tunatoa wito kwa wananchi wote kushikamana na kusimama imara katika kipindi hiki kigumu ili kulinda demokrasia.
Zitto Kabwe, MB
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Alhamisi, 23 Juni 2016.