Mtuhumiwa wa mauaji ya
aliyekuwa mwandishi wa habari wa Chanel Ten mkoani hapa, Daudi Mwangosi,
Pacificus Simoni ametoa ushahidi wake mbele ya mahakama na kuieleza
kuwa alilazimishwa kusaini ungamo mbele ya mlinzi wa amani bila kujua
nini kilichoandikwa.
Alidai kuwa baada ya kutoka kuhojiwa
kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) na Ofisa wa Makosa ya Jinai ya Mkoa
(RCO), akifananishwa na picha ya gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012
alipokana siyo yeye, alipelekwa kwenda kufanya ungamo kwa mlinzi wa
amani, Frola Mhelela ambaye alikuwa shahidi namba tatu.
Alidai wakati anakwenda kwa mlinzi wa
amani alisindikizwa na Staff Sajent Erick, ambaye alikuwa ameshika
bahasha na kumkabidhi kwa mlinzi huyo. Mtuhumiwa huyo alidai mlinzi huyo
alitoa karatasi na kuisoma kisha baadaye alimuambia aisaini, naye bila
kuhoji alisaini ile karatasi kwa sababu ilitoka kwa kiongozi wake ambaye
ni RCO, Nyegesa Wankyo.
Katika kesi hiyo wakili wa utetezi,
Rwezaura Kaijage aliiomba Mahakama kwamba mawakili wa upande wa Jamhuri
wataleta majumuisho ya mwisho leo.
Hata hivyo, upande wa jamhuri ambao
uliongozwa na wakili Sunday Hyera, ulisema hawana pingamizi lolote juu
ya upande wa utetezi baada ya kukaa na kukubalina kwa pande zote mbili
saa nane mchana watawasilisha majumuisho hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa,
Dk Paulo Kihwelo alisema Mahakama imekubali ombi la wakili wa utetezi
kuleta majumuisho, huku Juni 27 wakisikiliza maoni ya wazee wa baraza
kwa ajili ya kupanga hukumu.