Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Amos Makalla akikagua wachezaji wakati wa
Uzinduzi wa mashindano ya UMISETA ambayo mwaka huu yamedhaminiwa na
kampuni ya Coca Cola. Uzinduzi huo ulifanyika May 10, 2016 katika uwanja wa Sokoine ambapo kulifanyika michezo na burudani mbali mbali. .
Mashindano
kwa ajili ya fainali za kitaifa za Copa-UMISSETA ambayo yanadhaminiwa
na kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola, na ambayo yalipangwa kuanza
kufanyika siku ya leo hadi hapo tarehe 24 Juni 2016 yametangazwa
kuahirishwa. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya serikali iliyotolewa hapo
jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa), George Simbachawene, serikali imechukua uamuzi huo ili kupisha
utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la upatikanaji wa madawati, ambao
kikomo chake ni mwisho wa mwezi huu. Mashindano haya ya fainali za
Copa-UMISSETA yalilenga kuzikutanisha timu za mikoa mbalimbali nchini
kwa pamoja Jijini Mwanza, zikiwa zimeundwa na wachezaji mbalimbali
kutoka shule za sekondari ili wachuane kwenye michezo na sanaa.
Mkuu
wa Wilaya ya Temeke - Dar es Salaam, Sophia Mjema (kushoto),
akisalimiana na wachezaji wa timu ya Makongo Sekondari katika Mashindano
ya UMISETA ambapo kampuni ya Coca Cola ndiyo walikuwa ni wadhamini
wakubwa wa michuano hiyo kwa mwaka 2016. - “Thamira yetu katika
kudhamini mashindano haya na kushirikiana TAMISEMI iko pale pale, tukiwa
tumejidhatiti kuendelea kuunga mkono jitihada za kutambua na kuinua
vipaji vya vijana ambao watakuja kuifikisha Nyanja ya michezo nchini
katika kiwango cha juu zaidi. Tutaendelea kuunga mkono na kusaidia kukua
kwa sekta ya michezo nchini, hususani mashindano ya mpira wa miguu
pamoja na mpira wa kikapu kwa vijana,” alisema David Karamagi,
Mwakilishi Mkazi wa Coca-Cola Tanzania. Karamagi aliongeza kuwa kampuni
ya Coca-Cola Tanzania inayo imani ya dhati na ikiamini ya kwamba
mashindano ya michezo yanayoanzia ngazi ya chini kabisa ndiyo namna
thabiti nay a kipekee katika kuibua vipaji vya wachezaji nchini. Pia
Karamagi alisema kuwa, wakati wadau wakisubiri kwa hamu kutangazwa kwa
tarehe mpya za kurejewa kwa fainali za mashindano haya nchini, Coca-Cola
Tanzania ilishajipanga kudhihirisha ya kwamba michezo ni zaidi ya
ushindani, kwa kuweza kuambatanisha mashindano haya na kujenga
mshikamano wa timu shindani, urafiki na hata nidhamu kwa wachezaji na
timu za mikoa inayoshiriki. Hivyo basi, kwa udhamini ulioingiwa mwaka
huu, Coca-Cola Tanzania itaweza kupanua wigo wa ushirikishwaji wa
michezo murua zaidi mbali ya mpira wa miguu, hasa kwa kuweza kujumuisha
mpira wa kikapu. “Kampuni ya Coca-Cola nchini tutaendelea na dhamira
yetu ya kuunga mkono jitihada ya vijana mbalimbali nchini kote katika
kuwasaidia kudhihirisha vipaji vyao kupitia mashindano mbali mbali ya
michezo, ikiwa ni pamoja na UMISSETA na Copa Coca-Cola’” alimalizia
Karamagi.
