Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akisaini
leseni ya madini itakayoiwezesha kampuni ya Edenville International (T)
Ltd kuchimba makaa ya mawe katika eneo la Mkomolo na Namwele mkoani
Rukwa kwa ajili ya kuzalisha umeme. Wanaoshuhudia ni Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (wa pili kulia),
Kamishna Msadizi wa Madini anayeshughulikia Wachimbaji Wadogo, Julius
Sarota (wa kwanza kulia), Mwanasheria wa Wizara, Abbas Kisuju (kushoto
kwa Waziri) na Mhandisi Joseph Kumburu (kushoto kwa Mwanasheria).
Watendaji
kutoka kampuni ya Edenville (T) Ltd wakishuhudia Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kulia), akisaini leseni ya
madini itakayoiwezesha kampuni hiyo kuchimba makaa ya mawe katika eneo
la Mkomolo na Namwele mkoani Rukwa kwa ajili ya kuzalisha umeme wa kiasi
cha megawati 300. Kutoka kushoto mstari wa mbele ni Gwakisa Mwakyusa,
Cassiano Kaegele, Mohj Pryor na Peet Meyer.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akisisitiza
jambo mbele ya Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Taasisi na
kampuni ya Edenville (T) Ltd kabla hajasaini leseni inayoiruhusu kampuni
hiyo kuchimba makaa ya mawe katika eneo la Mkomolo na Namwele mkoani
Rukwa kwa ajili ya kuzalisha umeme wa megawati 300. Kikao hicho pia
kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini,
anayeshughulikia Sekta ya Madini, Profesa James Mdoe (hayupo pichani) na
Kamishna Msadizi wa Madini anayeshughulikia Wachimbaji Wadogo, Julius
Sarota (hayupo pichani).
Na Teresia Mhagama.
WAZIRI
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesaini leseni ya
madini itakayoiwezesha kampuni ya Edenville International (T) Ltd ambayo
ni kampuni tanzu ya kampuni ya Edenville Energy PLC ya nchini Uingereza
kuchimba makaa ya mawe katika eneo la Mkomolo na Namwele mkoani Rukwa
kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Utiaji
saini wa leseni hiyo ulifanyika jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa
Wizara ya Nishati na Madini na kushuhudiwa na watendaji mbalimbali wa
Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake wakiongozwa na Naibu Katibu
Mkuu anayeshughulikia Sekta ya Madini, Profesa James Mdoe pamoja na
watendaji wa kampuni ya Edenville.
Naibu
Katibu Mkuu, Profesa James Mdoe, alisema kuwa baada ya kupatikana kwa
leseni husika kampuni hiyo itaanza kazi ya kuchimba madini hayo ya makaa
ya mawe ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
“Baada
ya kuanza kuchimba makaa hayo mwezi Juni, kampuni hii imelenga kujenga
mtambo wa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 300 katika kipindi cha
kati ya miezi 20 hadi 22 baada ya kupata cheti cha mazingira kutoka
Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira,” alisema Profesa
Mdoe.
Alisema
kuwa umeme huo wa megawati 300 utazalishwa katika kipindi cha miaka 35
kwa kutumia hifadhi ya makaa ya mawe ambayo Kampuni hiyo imethibitisha
kuwepo katika leseni yao kwenye eneo la Mkomolo, mkoani Rukwa ambayo
yanafikia tani milioni 173.
Alieleza
kuwa kiasi hicho cha umeme kinaweza kuongezeka endapo watagundua
mashapo zaidi ya makaa ya mawe katika eneo lao lingine la Muze ambalo
linaonesha dalili ya kuwa na makaa ya mawe mengi na lipo karibu na eneo
la Mkomolo.
Naibu
katibu Mkuu alisema kuwa katika kikao hicho wamekubaliana na kampuni ya
Edenville kutekeleza masharti yote yaliyopo ndani ya leseni ikiwemo
kutekeleza kazi zote zilizopangwa kufanyika kama Mpango Kazi wa kampuni
hiyo unavyoelekeza.
“Tumewahimiza
waishi maneno yao, mfano hapa wameeleza kuwa wanatarajia kuanza
kuchimba makaa ya mawe mwezi Juni mwaka huu, inabidi watekeleze suala
hilo ili mwisho wa siku tufikie lengo la kuzalisha umeme wa kutosha
utakaowezesha nchi yetu kuwa na viwanda vingi ili Tanzania ifikie uchumi
wa Kati ifikapo mwaka 2025,” alisema Profesa Mdoe.
Aliongeza
kuwa Wizara itatoa ushirikiano kwa wawekezaji mbalimbali wanaojitokeza
kuwekeza katika Sekta za Nishati na Madini na ndio maana Waziri Muhongo
kuanzia mwanzoni mwa mwezi wa Pili mwaka huu amefanya mazungumzo na
makampuni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kusikiliza
mapendekezo yao kuhusu uwekezaji wa umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali
ikiwemo upepo, jua, maji, mawimbi ya bahari, makaa ya mawe, gesi asilia,
bayogesi na joto ardhi ambapo kampuni zaidi ya 300 zilijitokeza.
Naye
Mkurugenzi wa kampuni ya Edenville, Cassiano Kaegele, alimshukuru
Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano kwa
juhudi mbalimbali wanazofanya katika kuhakikisha kwamba miradi
mbalimbali inatekelezwa na kueleza kuwa kasi iliyopo sasa ikiendelea
miradi mingi itatekelezeka na Tanzania haitalazimika kununua umeme
kutoka nchi nyingine kwani ina vyanzo vya kutosha vya kuzalisha umeme
huo.
Naye
Peet Meyer, Mjiolojia kutoka kampuni hiyo ameeleza kuwa uchimbaji wa
makaa ya mawe katika maeneo hayo utafanyika kwa njia ya mgodi wa wazi
(opencast) katika miaka kumi ya kwanza na baadaye watachimba chini ya
ardhi na kwamba makadirio ya gharama za mradi ni Dola za Marekani
milioni 176. Leseni hiyo ya uchimbaji ni ya miaka kumi na kampuni ya
Edenville wanaweza kuihuisha tena baada ya miaka hiyo kupita.