Oct 13, 2015

MKAPA ATAKA MFUMO WA UN UBADILISHWE

IMG_6897
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez akipozi na bango la picha lenye rangi mbalimbali zinazowakilisha malengo ya dunia 17 kwa Maendeleo Endelevu wakati wa mdahalo kwenye juma la Umoja wa Mataifa ambalo linamalizika leo katika maadhimisho ya miaka 70 tangu kuundwa kwa umoja huo. Mdahalo huo umefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jana.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).

Na Mwandishi wetu
RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa ametoa wito wa kufanyika kwa mabadiliko katika mfumo wa uendeshaji wa Umoja wa Mataifa ili kukidhi mahitaji ya sasa ya dunia.
Mkapa alisema hayo jana katika mdahalo kwenye juma la Umoja wa Mataifa ambalo linamalizika leo katika maadhimisho ya miaka 70 tangu kuundwa kwa umoja huo. Mdahalo huo umefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jana.
Mkapa ambaye alichukua muda wake mwingi kuelezea na kuangalia maslahi ya Umoja wa Mataifa kwa dunia na changamoto inazokabiliana nazo, alisema kwa muda sasa dunia inataka mabadiliko katika uendeshaji wa Umoja huo lakini wanaonufaika na mfumo wa sasa wamekuwa wagumu kukubali mabadiliko.
Alisema kuna mambo sasa yanatokea yanayohatarisha usalama wa mataifa, lakini hatua zinazopendekezwa zinashindwa kuchukuliwa kutokana na kuendelea kuwapo kwa tabia ya vita baridi kati ya mataifa makubwa yenye kura ya veto katika umoja huo.
Alisema yeye anaungana na watu wengine duniani wanaotaka mabadilio katika Umoja huo yatakayozingatia jiografia za kisiasa duniani zinazoweza kusaidia kuinua uwezo wa utekelezaji wa Vyombo vya Umoja wa Mataifa likiwemo baraza Kuu na Baraza la Usalama.
IMG_6893
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez akipozi na Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mh. Fionnuala Gilsenan.
Alisema kwamba yapo baadhi ya mataifa na wakazi wa dunia hii ambao wanataka kuondolewa kwa kura ya turufu inayomilikiwa na mataifa kadha kutokana na makubaliano ya vita kuu ya pili ya dunia.
Alisema anafahamu kwamba Afrika inakubaliana na suala hilo kimsingi ingawa lina changamoto yake kwamba nini kitatokea kama kura hiyo ya turufu itaondolewa.

Hata hivyo, Mkapa alisema kwamba masuala ya usalama wa dunia ni nyeti sana kubaki katika mikono ya watu wachache na kutaka uwezo huo kupewa dunia kwa kuiwekeza katika sheria ya kimataifa inayotaka uwajibikaji wa pamoja katika masuala ya usalama.

Alisema katika kongamano hilo la vijana kwamba Afrika imepitisha azimio la pamoja Machi 8,2005 la kutaka mabadiliko makubwa katika vyombo vya Umoja wa Mataifa na umoja wenyewe.