Oct 10, 2015

MAGUFULI CUP YAZINDULIWA RASMI, ABAJALO YAANZA KWA USHINDI

TIMU ya Abajalo SC leo imeifunga timu ya Zakhem SC kwa bao 2-1 kwenye mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Magufuli Cup ‘#Hapa Kazi Tu’ iliyoanza kutimua vumbi rasmi leo kwa mchezo mmoja uliochezwa kwenye uwanja wa Mwl. Nyerere, Magomeni jijini Dar es Salaam.

 Magoli yote mawili ya Abajalo yamefungwa na Lameck Daiton, goli la kwanza limefungwa dakika ya tisa wakati goli la pili limefungwa dakika ya 11 kwa mkwaju wa penati baada ya Muhsin Said kuangushwa kwenye eneo la hatari wakati akielekea kufunga goli la pili.

 Goli pekee la Zakhem limefungwa na Muhsin Ngalanda kwa kichwa baada ya timu hiyo kutengeneza nafasi nzuri na Ngalanda kuitumia vyema nafasi hiyo kuukwamisha mpira wavuni na kuipa timu yake goli la kufutia machozi kwenye mchezo wao wa kwanza.

Mchezo huo wa ufunguzi ulikuwa ni mkali na wakuvutia uliokutanisha wachezaji wenye uwezo na vipaji vya hali ya juu ambapo umati mkubwa wa mashabiki walijitokeza kushuhudia pambano hilo.

Idd Azan ambaye ni mgombea Ubunge wa Jimbo la Kinondoni kwa tiketi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiye aliyezindua mashindano hayo akiongozwa na Madee ambaye ni msanii wa kundi la muziki la Tip Top Connections ambao ndio wandaaji wa mashindano hayo.

Azan amesema, mashindano hayo licha ya kutoa nafasi kwa vijana kuonesha vipaji vyao, lakini michuano hiyo ina lengo la kuwakumbusha wachezaji na wapenzi wote wa soka kupiga kura kwa amani kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 25 mwaka huu.

Mgombea huyo pia amelipongeza kundi la Tip Top Connections kwa kuandaa mashindano hayo hasa kwa kipindi hiki cha kampeni ili kuwaweka watu tofauti pamoja na kuwakumbusha kuhusu umuhimu wa kuchagua viongozi bora watakao watumikia kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Naye Madee kwa niaba ya Tip Top Connections amemshukuru Bw. Azan kwa kukubali kufungua mashindano ya Magufuli Cup na kuzungumza na vijana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi mkuu.

Michuano hiyo itaendelea tena Jumamosi (kesho) kwa timu za Tuamoyo na Burudani kuoneshana kazi kwenye uwanja wa Machava, Kigamboni.