Dodoma/Dar. Marais wastaafu watatu na makamu wa
zamani wa CCM jana walifanya kazi kubwa ya kukinusuru chama hicho
kuingia kwenye mgogoro uliokuwa unanukia baada ya Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa kuenguliwa kwenye mbio za urais.
Kwa mara ya kwanza, wajumbe watatu wa Kamati Kuu
ya chama hicho juzi walijitokeza hadharani na kupinga uamuzi wa chombo
hicho wa kupitisha majina ya wagombea kwa njia ambazo walisema
zinazokiuka katiba ya CCM.
Kama hiyo haitoshi, jana wajumbe wa Halmashauri
Kuu walimuweka mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kwenye hali ngumu
baada ya kuimba wimbo wa kuonyesha kuwa na imani na Lowassa, likiwa ni
tukio la kwanza la aina yake kwenye vikao vya juu vya chama na ambalo
liliashiria kuanza kupoteza utii kwa chama.
Habari kutoka ndani ya NEC zinasema kuwa baada ya
mapumziko ya chakula cha mchana, kikao hicho kilijadili kwa kirefu
sakata la kuchujwa kwa Lowassa na pande zinazohusika zilizungumza kwa
hisia kali, ndipo marais hao, Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Abeid
Amani Karume na makamu mwenyekiti wa zamani, John Samuel Malecela
walipolazimika kuingilia kati.
“Ilibidi kwanza wote waliokuwa wanagombea urais
waondolewe kwenye mkutano ndipo tuanze kujadiliana,” alisema mmoja wa
wagombea ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Mjumbe mwingine wa kikao hicho alisema Malecela,
Mkapa, Karume na Mwinyi walitumia maneno ya busara na kuwatahadharisha
wajumbe dhidi ya misimamo yao.
“Walituonya kuhusu kujali masuala yetu binafsi
kuliko amani ya nchi na kututaka kuangalia sana misimamo yetu kwa kuwa
inaweza kuhatarisha amani,” alisema mjumbe huyo.
Alisema wakati kikao kilipositishwa kwa ajili ya
chakula cha mchana, kuna baadhi ya wajumbe waliondoka eneo hilo na
wengine kubaki, akiwamo Lowassa ambaye hakujulikana alielekea eneo gani
kwenye jengo hilo.
Kikao cha mchana kilianza bila ya Lowassa kuwamo
na Karume alianza kuzungumza, na kufuatiwa na Malecela, Mkapa, na
Mwinyi, ambaye alipomaliza aliwashauri wajumbe kuwa waendelee na upigaji
kura kwa kuwa suala hilo limeshaeleweka.
Mkutano ulipoanza kupiga kura ndipo Lowassa
alipoingia na kukuta kazi ya upigaji kura inaendelea na hivyo kuendelea
na shughuli hiyo.
Awali, kwa mara ya kwanza, Kikwete jana alikumbana
na mapokezi ya aina yake wakati wajumbe walipomuonyesha waziwazi
kupinga uamuzi wa Kamati Kuu kwa kuimba wimbo wa kumuunga mkono Edward
Lowassa kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu kuanza.
Hali hiyo imetokea wakati baadhi ya wanachama wa
CCM wakiwa bado hawajakubali kuenguliwa kwa Lowassa kwenye
kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya CCM baada ya Kamati Kuu kupitisha
majina ya John Pombe Magufuli, Amina Salum Ali, Bernard Membe, January
Makamba na Dk Asha Rose Migiro kwa ajili ya kupigiwa kura Halmashauri
Kuu.
Hali ya kutoafikiana na uamuzi huo wa Kamati Kuu pia ilionekana
nje ya jengo la makao makuu ya CCM, ambako kikundi cha watu ambao baadhi
yao walivalia sare za CCM kiliimba jina la Lowassa wakati wajumbe
wakiingia kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu.
Wakati Kikwete akiongoza viongozi wa juu kuingia
kwenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kuendesha kikao cha Halmashauri
Kuu, wajumbe walipaza sauti zao kuimba “tuna imani na Lowassa, oyaa,
oyaa, oyaa. Lowassa kweli? kweli kweli kweli Lowassa...”.
Rais Kikwete na viongozi wenzake walisita kuingia
ukumbini, lakini baadaye aliingia katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
akifuatiwa na Kikwete, makamu mwenyekiti wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein na wa Bara, Phillip Mangula.
Wimbo huo uliongozwa na kundi lililokuwa nyuma
ukumbini likijumuisha mfanyabiashara maarufu nchini, Christopher
Gachuma, mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mara, Christopher Sanya, aliyekuwa
mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo na mjumbe mwingine
aliyetambulika kwa jina la Joseph Marwa ambaye anatoka Mara. Wajumbe hao
na baadhi wengine waliendelea kuimba wimbo huo kwa takriban dakika
mbili kabla ya kunyamaza kumruhusu Kikwete afungue kikao.
“Kweli Haijawahi kutokea,” alisema Rais Kikwete
akionekana kusawajika. Na wajumbe walimjibu, “kweli”. Akawauliza tena,
“habari za asubuhi” na kujibiwa,”nzuri”.
Kinana alisimama na kutangaza akidi kwamba idadi
ya wajumbe inatakiwa kuwa 325 lakini waliohudhuria ni 274, sawa na
asilimia 87, hivyo akidi imetimia.
Ndipo Kikwete alipoeleza ajenda za kikao hicho na jinsi kitakavyoendeshwa na akamaliza kwa kuwataka wajumbe wapunguze jazba.
“Matumaini yangu ni kwamba vikao vitakwenda
vizuri, tutazungumza kwa utulivu. Tupunguze jazba. Unajua ukikasirika
wakati mwingine hoja hazitoki sawasawa, kwa hiyo matumaini yangu makubwa
ndiyo hayo. Ninawatakia kikao chema,” alisema Rais Kikwete.
Afungua kikao
Akifungua kikao hicho, Rais Kikwete alisema mkutano huo una ajenda tatu.
“Karibu katika Mkutano wa Halmashauri Kuu Maalumu,
kwa mujibu wa katiba yetu chama. Kikao hiki kitakuwa na ajenda; kupokea
mapendekezo ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020; Kufuta kifungu cha
kanuni kinachoweka ukomo wa ubunge na madiwani wa viti maalumu,
mtakumbuka tulikuwa tumeweka ukomo wa vipindi viwili na sasa
tunapoelekea kwenye mchakato wa Katiba Inayopendekezwa na haijapita,
tumeona tufungue hiki kifungu ili itakapokuja Katiba mpya, basi tuwe
tunafuata hayo ya Katiba Mpya yanayopendekezwa ya 50:50,” alisema
Kikwete.
Aliongea kuwa baada ya hapo itafuata ajenda ya
kuchagua mwanachama anayependekezwa kugombea urais Zanzibar na mgombea
urais wa Tanzania.
Baada ya kusema hayo, aliwataka waandishi wa habari kutoka
ukumbini ili kikao kiendelee. Baadhi ya wajumbe walianza kuwasili kwenye
eneo la jengo hilo wakiwa wamenuna na baadhi kupiga kelele kuwa kikao
cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ni chao hivyo wangeweza kubadilisha
uamuzi wa Kamati Kuu.
Nje ya ofisi hizo za makao makuu ya chama hicho kulikuwa na mshikemshike baina ya wafuasi wa Lowassa na polisi.
Mapema asubuhi kabla ya wajumbe wa Halmashauri
Kuu kuingia kwenye kikao, hali ilikuwa shwari na watu walikuwa kwenye
makundi wakizungumzia matokeo ya mchujo wa wagombea urais.
Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)
walikuwa wamekaa ndani ya magari yasiyopungua matano kusimamia hali ya
usalama wakati wajumbe wakiingia eneo hilo.
Barabara Kuu inayopita mbele ya jengo la makao
makuu ya CCM ilifungwa kuanzia katika makutano na Barabara ya Mbeya
karibu na ofisi za mkoa za Mamlaka ya Mapato (TRA) na mwanzoni mwa
bustani ya Nyerere Square katika Barabara ya Lindi.
Kutokana na kufungwa barabara hiyo, foleni ndogo
ilianza kwenye barabara za ndani iliyokuwa ikitengenezwa na magari ya
wajumbe wa mkutano mkuu waliokuwa wakishuka eneo hilo kuchukua vifaa na
daladala zilizokuwa zikifanya safari zake kati ya Jamatini na maeneo
mengine ya mji.
Eneo lote linalozunguka ofisi za CCM zilijaa
makada na wakazi waliokuwa wakipita kushuhudia wafuasi wa Lowassa
waliokuwa wakipigania ‘haki’ ya kada huyo kubakizwa kwenye mchakato wa
urais.
Saa 6:20 mchana, kikundi kidogo cha makada
waliojiita wafuasi wa Lowassa kilianza kuimba “Lowassa, Lowassa.
Tunamtaka Lowassa wetu”.
Kikundi hicho kilizidi kukua na kuendelea kuimba
kikiwa ndani ya uzio wa bustani ya Nyerere Square na kuvutia idadi kubwa
ya watu na waandishi huku gari tatu za polisi zikiwa jirani kufuatilia
mwenendo wao.
“Siku hizi tunakwenda na matakwa ya wananchi. Zama
za kusema chama kwanza zimepitwa na wakati… lazima uwapatie wananchi
mtu wanayemtaka. Huu siyo wakati wa chama kimoja ni wa vyama vingi ni
lazima twende na nyakati na mahitaji ya sasa,” aling’aka mtu
aliyejitambulisha kwa jina la Michael William (65) aliyedai alijiunga na
CCM tangu 1963.
Makada hao walienda mbali zaidi kudai uamuzi wa kumuengua Lowassa unaua chama hicho na kutishia kurejesha kadi za uanachama.
Baada ya nusu saa kundi hilo liliongezeka na
kutoka nje ya uzio hadi karibu na Barabara ya Nyerere mkabala na ofisi
za CCM ambako polisi walikuwa wamefunga barabara, na kutoa kashfa kwa
viongozi wa chama hicho.
