Dar es Salaam. Mvutano mkali ulioibuka jana
katika kikao cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25, umesababisha kushindwa kumtaja mgombea wake wa urais.
Kutokana na mvutano huo, viongozi wa vyama hivyo
waliahirisha kikao hicho na kuitisha mkutano na waandishi wa habari na
kueleza kuwa watamtangaza mgombea huyo Jumanne ijayo.
Kikao hicho kilichowahusisha wabunge wote na
viongozi wakuu wa vyama vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi
vinavyounda Ukawa, kilifanyika jana katika ukumbi wa Millenium, Dar es
Salaam.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alishindwa kuwaeleza wanahabari kilichowakwamisha kumtangaza mgombea,
huku akisisitiza kuwa wanataka kuweka mambo sawa.
“Hatuwezi kuwaangusha Watanzania na kipindi hiki
ndiyo chetu kwani tunaingia katika uongozi wa Serikali ili kulikomboa
taifa,” alisema: “Kuna mambo ya kukubaliana na kuweka sawa, tutamtaja
mgombea wetu Julai 14 (keshokutwa). Naomba niwaeleze Watanzania kuwa
Ukawa haiwezi kuvunjika tunachokifanya ni kuwa makini katika maamuzi
yetu.”
Alisema kikao cha Kamati ya Ukawa kilifikia
muafaka na jana kuwasilisha mrejesho kwa wabunge ndipo ulipofikiwa
muafaka wa kusubiri hadi keshokutwa, huku akisisitiza kuwa katika
kugawana majimbo wamekubaliana kwa asilimia zaidi ya 90.
Alipobanwa aleleze ni mambo gani yaliyokwamisha
kufikiwa kwa muafaka alisema: “Kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama
vyetu ila hayawezi kuleta matatizo, tupo pamoja na tutatoa jibu la
pamoja.”
Alisema Ukawa imetokana na maoni ya wananchi
kuhusu Katiba Mpya, hivyo kiongozi atakayepitishwa na chama hicho lazima
awe, mwadilifu, muwazi na mwajibikaji.
“Lazima tuwe na mgombea atakayesimamia mambo ya
wananchi waliyotaka yawemo katika Katiba, mambo hayo ni yale yaliyowekwa
katika rasimu ya Katiba ya Jaji (Joseph) Warioba,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema kama katiba ya nchi ingekuwa na kifungu
kinachoruhusu vyama kuungana, vyama vinavyounda Ukawa vingeungana lakini
kutokana na sintofahamu hiyo katika Katiba, wanalazimika kutatua
changamoto hiyo kwa umakini mkubwa.
Kuhusu majimbo alisema; “ni kama tumeshagawana
yote isipokuwa ambayo yana wagombea wawili wawili, yaani kutoka vyama
zaidi ya viwili. Tumekubaliana majimbo zaidi ya 170 mpaka sasa.”
Imeelezwa kuwa katika kikao hicho kilichoanza saa tisa alasiri
mvutano ulikuwa kati ya viongozi wa juu wa CUF dhidi ya wabunge na
viongozi wengine wa vyama vyote vinavyounda Ukawa, wakiwamo wa CUF.
Habari hizo zilieleza kuwa viongozi wa CUF
wanashinikiza mgombea urais wa Ukawa awe Profesa Lipumba, huku wabunge
wa Ukawa wakimtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwa maelezo
kuwa anakubalika zaidi.
“Unajua Lipumba anataka kugombea urais wakati
akitambua wazi kuwa upande wa Zanzibar pia CUF inasimamisha mgombea
urais. Wajumbe wa Ukawa wanataka Chadema isimamishe mgombea upande wa
Bara na kuiachia CUF Zanzibar,” zilieleza taarifa hizo.
Ilielezwa kwamba viongozi wa juu wa CUF, wakiwamo
kutoka Zanzibar wametoa baraka zote kwa Dk Slaa kugombea, lakini kikwazo
kimebaki kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaomuunga mkono
Profesa Lipumba.
“Nakwambia wazi muafaka hautapatikana na kikao
hiki kitaahirishwa hadi Julai 14 au 15 maana huko ndani hakuna
maelewano, kikubwa ni urais tu huko katika majimbo hakuna shida,”
zilieleza taarifa hizo.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho ni
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Dk Slaa, Mwenyekiti wa NLD, Dk
Emmanuel Makaidi, Profesa Lipumba, Katibu Mkuu wa NCCR, Mosena Nyambabe,
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya.
chanzo: MWANANCHI
