Wakati Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari akiupunguza mshahara
wake muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka huu, marais wengine
wa Afrika wameonekana kujilimbikizia mishahara mikubwa, tofauti na
pato ‘kiduchu’ la wananchi wao kwa mwaka.
Kwa mujibu
wa uchambuzi wa mtandao wa African Review, marais watano wanaoongoza kwa
kuwa na mishahara mikubwa kwa mwaka ni Rais Paul Biya wa Cameroon
anayelipwa Dola za Marekani 610,000, akifuatiwa na kiongozi wa Morocco,
Mfalme Mohammed VI anayelipwa Dola 480,000 na Rais Jacob Zuma wa Afrika
Kusini ni wa tatu akilipwa Dola 272,000.
Rais Jakaya
Kikwete ni wa nne kwa malipo ya Dola 192,000 na wa tano ni Rais Abdel
Aziz Bouteflika wa Algeria, anayelipwa Dola168,000.
Mtandao
huo umebainisha pato la Mtanzania wa kawaida kwa mwaka kuwa ni Dola
1750 sawa na Sh3.5 milioni, linalozidiwa mara 114 na kiasi anacholipwa
Rais kwa mwaka.
Madhumuni ya utafiti wa mtandao huo
ilikuwa kuangalia kiasi wanacholipwa marais wa Afrika kwa mwaka na kile
inachopata taifa husika kwa muda huo.
Pia walilenga kuangalia uhusiano wa viongozi hao na wananchi wa kawaida wanaowangoza.
Kwa
mujibu wa mtandao huo, vyanzo vya taarifa za mishahara ya marais hao
vilipatikana kutoka mitandao na wanahabari wa nchi husika.
Tofauti
na maraisi wengine, Rais mpya wa Nigeria, Muhammadu Buhari, alitangaza
punguzo la mshahara wa rais pamoja na wafanyakazi wengine wa Serikali
mara alipoingia madarakani.
Rais mwingine aliyefanya
hivyo ni Uhuru Kenyatta wa Kenya, ambaye pamoja na makamu wake
walipunguza mishahara yao kwa asilimia 20 baada ya kuingia madarakani
mwaka 2013.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo marais wa nchi
zilizoendelea bado wanapata mshahara mkubwa, ingawa unaendana na kipato
cha mwananchi wa kawaida kwa mwaka.
Kwa mfano, Rais
Barack Obama wa Marekani anapata mshahara wa Dola 400,000 kwa mwaka.
Stephern Harper wa Canada, Dola 260,000 na Angela Merkel wa Ujerumani,
Dola 234,000.
Rais wa zamani wa Tunisia, Moncef
Marzouk, baada ya kukumbwa na mgogoro wa kiuchumi, alitangaza punguzo
la robo tatu ya mshahara wake kwa mwaka kutoka Dola 176, 868 hadi Dola
58,956.
Kitendo cha Rais Marzouk, Buhari na Kenyatta
kimeonekana ni tofauti na marais wengine ambao huongeza mishahara yao
baada ya kuingia madarakani.
Kwa mfano, Rais wa Misri
alijiongezea mshahara kutoka Dola 280 kwa mwezi, kiwango ambacho
kiliwekwa na rais wa awali Mohammed Morsy hadi Dola 5,900 kwa mwezi.
Hata
hivyo katika nchi nyingine, viongozi huchukua pato la nchi kwa ajili ya
matumizi yao binafsi. Kwa mfano nchini Morocco, Dola 1 milioni hutumika
kwa siku kwa ajili ya makazi 12 ya kifalme ya Mfalme Mohammed VI na
makazi yake mengine binafsi 30.
Wakati huo, Dola7.7
milioni hutumika kwa ajili ya magari ya kifalme na Dola 40,000 kwa
ajili ya mshahara wa mwezi kwa wafanyakazi wa makazi ya kifalme.
Mwaka
2014, Mfalme Mswati wa Swaziland, alijiongezea bajeti yake, ambayo
inajumuisha mshahara na wanafamilia wake kwa asilimia 10. Aliongeza
Dola 61 milioni kwa kunyofoa kiwango kikubwa cha bajeti kuu ya Serikali
yake ya kifalme.
Hata hivyo, kulingana na masharti ya nchi za kifalme, ongezeko hilo huwa halijadiliwi bali huwa sheria moja kwa moja.
Marais
wengine hujitengea mishahara midogo machoni mwa umma, lakini
wanafamilia wao humiliki biashara au kampuni nyingi. Kwa mfano, Rais
Eduardo dos Santos wa Angola, anapokea mshahara wa Dola 5,000 lakini
anaaminika kumiliki kiasi kikubwa cha utajiri kwenye viwanda vya mafuta,
huku wanafamilia wake pia wakimiliki viwanda hivyo.
Katika
nchi ya Guinea Equator, licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na
idadi ya watu chini ya milioni moja, bado nchi hiyo inatajwa kuwa na
pato la juu la nchi. Hata hivyo kiasi kikubwa cha utajiri huo
kinamilikiwa na watu wachache na familia ya rais.
Kitengo
cha Sheria cha Marekani kilimshtaki mtoto wa kwanza wa Rais wa
Equatorial Guinnea, Teodoro Nguema Obiang Mangue, kwa kutumia Dola 315
milioni kununua nyumba na bidhaa nyingine za kifahari kati ya mwaka
2004 na 2011, licha ya kuwa ni waziri wa nchi hiyo anayelipwa chini ya
Dola 100,000 kwa mwaka.
Uchambuzi wa Africa Review
ulipochambua tena mishahara ya viongozi hao kwa kuulinganisha na pato la
nchi kwa mwaka, bado marais Paul Biya wa Cameroon, Ellen Johnson
Sirleaf wa Nigeria, Jakaya Kikwete, Peter Mutharika wa Malawi na Joseph
Kabila wa Congo walibainika ndiyo wanaolipwa mara 100 zaidi ya mapato ya
mataifa yao kwa mwakachanzo MWANANCHI
