
RIPOTI ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu kuchotwa kunakodaiwa isivyo halali kwa fedha katika Akaunti ya Escrow, sasa haitajadiliwa bungeni.
Naibu
Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana
alipokuwa akijibu Mwongozo wa wabunge kuhusu kujadiliwa kwa ripoti za
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Takukuru kuhusu
sakata hilo.
Mwongozo
wa awali kwa suala hilo ulitolewa na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje
(Chadema) aliyehoji kutoonekana kwa ripoti ya Takukuru katika ratiba ya
vikao vya Bunge na badala yake kuonekana ripoti ya CAG.
Kwa
mujibu wa ratiba mpya ya Bunge iliyotolewa juzi, inaonesha kuwa ripoti
ya CAG kuhusu sakata hilo la fedha katika akaunti ya Escrow,
itawasilishwa katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo
Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema),
Novemba 26, mwaka huu.
Akijibu
Mwongozo huo wa Wenje na baadaye wa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari (Chadema), kuhusu kwa nini ripoti ya Takukuru haitaletwa
kujadiliwa bungeni, Ndugai alisema kwa mujibu wa sheria, Takukuru
hawapaswi kuwasilisha ripoti yao bungeni.
“Waheshimiwa
wabunge Takukuru wao wakimaliza kazi yao, na wakibaini kuna makosa ya
jinai, inachukua hatua moja kwa moja kwa kuwasiliana na DPP (Mkurugenzi
wa Mashitaka) na kuwafikisha wahusika mahakamani,” alisema Ndugai.
Aidha,
Naibu Spika huyo akijibu hoja za wabunge hao kwamba kuna usiri na
kampeni zinafanywa katika kushughulikia suala hilo tangu lilipotua
bungeni, alisema hakuna usiri wowote unaofanywa kwani hatua
zinazochukuliwa ni zile zilizofikiwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge
ilipojadili sakata hilo.
Alisema
kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, ripoti hiyo ni lazima ipite kwenye
Kamati ya PAC kabla ya kujadiliwa bungeni, na kwamba kupangwa kwa kikao
hicho mwishoni mwa shughuli za Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge unaoendelea
ni utaratibu wa kawaida.
“Waheshimiwa
wabunge kitendo cha suala hili la Escrow kupangwa tarehe hiyo ni suala
la kawaida kwa shughuli za kibunge. Kama mnavyofahamu kwa kawaida Bunge
huanza kwa kujadili shughuli za serikali na zile za kamati huwekwa
mwishoni mwa vikao vyetu,” alisema Ndugai.
Hata
hivyo, hatua ya ripoti hiyo ya Takukuru kutangazwa kutowasilishwa
bungeni kulimfanya Zitto kusimama na kueleza kuwa ili Kamati yake iweze
kufanya kazi ipasavyo katika kuipitia ripoti ya CAG ni lazima ripoti
hiyo iambatane na ripoti ya Takukuru.
Hatua
hiyo ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu anayekaimu
nafasi ya Waziri Mkuu bungeni, Profesa Mark Mwandosya kusimama na
kulieleza Bunge kuwa Kamati ya PAC ina mamlaka ya kuwaita Takukuru
wakati itakapokuwa inajadili ripoti ya CAG.
Alisema
kimsingi si kwamba serikali inazuia kuwasilishwa kwa ripoti ya
Takukuru, bali suala hilo linatokana na matakwa ya kisheria, lakini
akasema Takukuru wanaweza kuwasilisha kwa Kamati ya Bunge aina nyingine
ya ripoti itakayosaidia kamati kufanya kazi yake kikamilifu.
NA MPEKUZI HURU.COM