HALI ya afya ya Rais Jakaya Kikwete imeendelea kuimarika kwa kasi na jana alizungumza kwa simu na uongozi wa juu wa Tanzania kwa mara ya kwanza tangu afanyiwe upasuaji wa tezi dume Jumamosi iliyopita.
Alizungumza
na Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali
Mohammed Shein na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, lakini pia alikuwa
anawasiliana na mamia kwa mamia ya wananchi na kujibu ujumbe mfupi wa
maandishi (SMS) wa kumpa pole, kumtakia heri na nafuu ya haraka, ambao
amekuwa anatumiwa na wananchi tangu mwishoni mwa wiki.
Tangu
alipofanyiwa upasuaji wa tezi dume Jumamosi iliyopita kwenye Hospitali
ya Johns Hopkins, Baltimore, Jimbo la Maryland, Marekani, Rais Kikwete
amepokea mamia kwa mamia ya SMS zikimpa pole na kumtakia nafuu ya
haraka.
Rais
Kikwete bado anaendelea kujibu SMS hizo za wananchi ambao wamemtumia.
Wenye SMS hizo wametakiwa kuendelea kusubiri majibu yake kwa sababu
anakusudia kujibu SMS zote ambazo ametumiwa.
Katika
hatua nyingine, madaktari wanaoendelea kumtibu Rais Kikwete, jana
waliondoa bendeji kwenye sehemu ambako alifanyiwa upasuaji, wakieleza
kuwa hali yake inaendelea vizuri na anapata nafuu kwa kasi nzuri.
Italia yaguswa
Nayo
Serikali ya Italia imemtakia afya njema Rais Kikwete na kumuombea apone
haraka na arejee katika shughuli zake mapema baada ya upasuaji wa tezi
dume mwishoni mwa wiki.
Salamu
hizo zimewasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi na
Balozi wa Italia nchini, Luigi Scotto wakati alipomtembelea Mkuu wa Mkoa
ofisini kwake, ambapo pia alipata fursa ya kutembelea Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Balozi
huyo alisema Serikali ya Italia imeguswa na afya ya Rais Kikwete na
inamtakia apone haraka ili arejee katika kuendeleza harakati za
kuwatumikia wananchi wake.
Pia
alisema Italia itaendelea kuisaidia Tanzania katika miradi yote
inayofadhiliwa na Serikali ya nchi hiyo, ikiwemo Mradi wa afya wa
magonjwa yanayoambukizwa hususani Ukimwi na Kifua Kikuu kupitia kwa
wajawazito yaani “Afya ya mama na mtoto” mradi unaofanyika katika
Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma na Kituo cha Afya cha Makole.
Akipokea
salamu hizo kwa niaba ya serikali, Dk Rehema Nchimbi, alimpongeza
Balozi wa Italia na serikali yake kwa moyo wa kiungwana na upendo kwa
watu wa Tanzania na hasa kutokana na kuguswa na afya ya Rais Kikwete.
Pia,
aliishukuru serikali ya Italia kwa misaada mingi inayoisaidia Tanzania
hususani kupitia Mradi wa afya ya Mama na Mtoto, misaada ya elimu na
matibabu ya magonjwa yanayoambukiza kupitia wajawazito.
