Katibu Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo akiongea
na wahusijka wa Kampuni ya Kajala Entertainment wakati alipofanya nao
mkutano leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapa
Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu ya Mbwa Mwitu.
Mkurugenzi
wa Kampuni ya Kajala Entertainment, Kajala Masanja akijitetea mbele ya
Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania wakati aliitikia wito wa Ofisi ya Bodi
hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu ya Sheria na
Kanuni zilizokiukwa katika filamu yake ya Mbwa Mwitu.
Mkurugenzi wa
Kampuni ya Kajala Entertainment, Kajala Masanja akiweka sahihi ya
kukubali kufanya marekebisho katika filamu yake pamoja na malipo ya
faini mbele ya Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania wakati aliitikia wito
wa Ofisi ya Bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu
ya Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu yake ya Mbwa Mwitu.
Meneja ambaye pia
ni Mratibu wa Kampuni ya Kajala Entertainment, Bi. Leah Mwendamseke
akiweka sahihi katika fomu maalum ya kukubali kufanya marekebisho katika
filamu iliyokaguliwa na Bodi hiyo mbele ya Katibu wa Bodi ya Filamu
Tanzania wakati aliitikia wito wa Ofisi ya Bodi hiyo leo jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu ya Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika
filamu ya Mbwa Mwitu.
Katibu Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo akiagana
na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajala Entertainment wakati alipofanya naye
mkutano leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapa
Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu ya Mbwa Mwitu.(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA, MAELEZO-DSM)
Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
BODI ya Filamu Tanzania
imezitaka Kampuni za filamu nchini kufuata Sheria na Kanuni mbalimbali
wakati wa kutengeneza filamu ili kuepusha ukiukwaji wa Sheria na Kununi.
Rai hiyo imetolewa leo na Katibu
wa Bodi hiyo, Bi Joyce Fissoo wakati alipofanya mkutano na Kampuni ya
Kajala Entertainment ambapo mnamo Septemba 22, mwaka huu ilikagua Filamu
fupi ya kampuni hiyo iliyopewa jina la Mbwa Mwitu yenye dakika 12 na
kubaini baadhi ya makosa.
Akiongea wakati wa mkutano na
wadau wa kampuni hiyo, Bi Fissoo alisema kuwa Bodi iliielekeza Kajala
Entertainment kuifanyia marekebisho filamu hiyo katika dakika ya 7
ambapo ilionekana wanawake wakidhalilishwa na kubakwa kinyama na pia
katika dakika ya 11 ambapo ilionyesha wizi na uvamizi.Alisema kuwa, wahusika
walielekezwa kufanya marekebisho hayo kwa kuondoa vipande husika na
baada ya kufanya marekebisho hayo waliwasilisha Bodi ya Filamu nakala ya
filamu iliyokuwa imefanyiwa marekebisho yenye dakika 12 na kupewa
kibali namba 4261 ya tarehe 24 Septemba, 2014.
Bi Fisso aliongeza kuwa, mnamo
tarehe 25 Septemba, 2014 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es
Salaam, filamu hiyo fupi ilionyeshwa bila ya kuzingatia marekebisho
yaliyokuwa yameelekezwa kwa mujibu wa Sheria kwa kuzingatia kifungu cha
Sheria cha 19 (2) (a).
“Baada ya ukiukwaji wa Sheria
katika kifungu cha 19 (2) (a) na kile cha 24 (i), (m) na (n) vya Kanuni
za Sheria ya Filamu husika, wahusika waliitwa mara mbili kufika Bodi ya
Filamu lakini hawakufanya hivyo, lakini baada ya kumbushio na kalipio
wahusika baadaye walifika Ofisi za Bodi katika kikao cha tarehe 13
Novemba mwaka huu”, alisema Bi. Fissoo.
Alieleza kwamba, wahusika
walikiri kuwa walipata ujumbe wa wito wao wa kuitwa na Bodi hiyo ambapo
Mratibu wa masuala yote ya Kampuni ya Kajala Entertainment, Bi. Leah
Mwendamseke aliieleza Bodi kuwa anaomba asamehewe kwa kuwa walikuwa na
shughuli nyingine mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni hiyo,
Kajala Massanja aliiomba radhi Bodi ya Filamu Tanzania huku akisema
kuwa mara nyingi yeye huwa amekuwa akiwaachia wsaidizi wake kutekeleza
majukumu ya kampuni yake ingawa yeye kama mmiliki wa kampuni hiyo
anawajibika moja kwa moja.
Aidha, Bodi iliitaka Kajala
Entertainment kueleza sababu ya kukiuka maelekezo ya Bodi ambayo
yalikuwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake licha ya mtunzi na
mwandishi wa musuada na muongozaji wa filamu hiyo, Bi. Leah Mwendamseke
alijitetea kuwa alifanya utafiti na kukutanana vijana mbalimbali
waliowahi kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo, Leah Mwendamseke
alishindwa kuoanisha uhalisia wa matokeo ya utafiti wake na ujenzi wa
visa vya hadithi ya filamu ambayo inaweza kupeleka ujumbe chanya kwa
jamii, huku wahusika wakieleza kwamba lengo lao kubwa lilikuwa ni
kuelimisha jamii kuhusu maovu yanayotokea na namna ya kuyaepuka ambapo
mtunzi huyo aliahidi kurekebisha vipengelee husika katika filamu hiyo
ili kuwa na filamu bora.
Kwa upande wake Mwakilishi toka
Ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Tanzania, Sylivester Mganga aliushauri
uongozi wa Kajala Entertainment kufuata maelekezo na kuzijua Sheria
mbalimbali zinazohusu mambo ya filamu kwa kuvishirikisha vyombo vya
ulinzi na usalama kabla ya kujichukulia maamuzi ya kutengeneza filamu
zenye kutishia amani ya nchi.