
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemruhusu Prashant Patel kubadilisha hati ya madai katika kesi aliyoifungua dhidi ya mshirika wake, Hashim Lundenga.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Frank Moshi,
amemruhusu Patel kupitia wakili wake Benjamin Mwakagamba wa kampuni ya
Uwakili ya BM, baada ya kuiomba mahakama hiyo kufanya hivyo ili aweze
kuingiza gharama ambazo zilijitokeza baada ya kufanyika kwa shindano la
Miss Tanzania, Oktoba 11, 2014.
Hata hivyo Hakimu Moshi alimtaka Patel kufanya
mabadiliko ya hati hiyo ya madai dhidi ya Lundenga na kuiwasilisha
mahakamani hapo kabla ya jana Jumatano.
Baada ya kuruhusu Patel kubadilisha hati hiyo ya madai, Hakimu huyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 3 kwa ajili ya kutajwa.
Patel amechukua hatua hiyo baada ya maombi yake ya
kutaka kuzuia shindano hilo la Miss Tanzania lililofanyika katika
Ukumbi wa Mlimani City, Jumamosi ya Oktoba 11, 2014 kushindikana.
Mshiriki huyo mwenza wa Lundenga kupitia wakili
Mwakagamba, waliyafungua maombi hayo ya kuomba zuio hilo la shindano la
Miss Tanzania chini ya hati ya dharura.
Katika maombi yake, Patel anadai Lundenga alikuwa
na mpango wa kuendesha shindano hilo kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar
es Salaam, kinyume cha sheria na bila hata ya kumwarifu.
Hivyo aliiomba mahakama itoe zuio la kufanyika kwa
shindano hilo hadi shauri la msingi alilofungua litakaposikilizwa na
kutolewa uamuzi.
Katika kesi yake ya msingi, Patel anadai pamoja na
mambo mengine, utekelezaji wa makubaliano ya Februari 20, 2012 na
malipo ya Sh19 milioni ambayo hayajalipwa kwa mujibu wa mkataba wao na
faida nyinginezo ambazo zimejitokeza hadi Septemba 23, mwaka huu.
Kupitia hati yake ya kiapo inayounga mkono maombi
yake, Patel anadai kuwa yeye na Lundenga ndio waanzilishi, waongozaji na
waendeshaji wa mashindano ya Miss Tanzania na wamekuwa katika hali hiyo
kwa miaka 20 sasa, tangu yaliporuhusiwa tena 1994.