Siku hizo, sikuwa na marafiki wengi, idadi kubwa ya marafiki ambao nilikuwa nao, kama kawaida walikuwa wavulana. Unaweza kujiuliza kwa nini nilikuwa nikipenda sana kuwa na marafiki wa kiume toka shule ya msingi mpaka ya sekondari, ila kiukweli ni kwamba nilitaka kuwa huru, sikutaka kuwa na wasiwasi.
Wavulana walikuwa watu ‘smart’ sana, unapokuwa karibu nao, unajihakikishia kwamba hakuna jambo baya ambalo litaweza kutangazwa, hata kama ulifanya kitu fulani ambacho kinaonekana kuwa kituko na ukawaomba wasiseme, ni kweli walikuwa wakikaa kimya, hicho kilinifanya niwatafute marafiki wa kiume zaidi.
AWAKERA WASICHANA, KISA WAVULANA
Masomo yalikuwa magumu, lugha ilikuwa ngeni na ndiyo ambayo ilinifanya kila siku niendelee kujifunza. Kipindi cha kwanza ilikuwa shida sana, kuzishika herufi na kuzungumza lilikuwa jambo gumu mno.
Kiukweli nilitamani kuzungumza lugha hiyo, wapo baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa na vichwa vyepesi sana ambao wala hawakuchukua muda mrefu kuifahamu lugha hiyo, tofauti na mimi.
“Bado tu,” aliniambia msichana mmoja. “Bado nini?” “Unaendeleza tabia yako mbaya,” aliniambia huku akionekana kukasirika. “Tabia gani?” niliuliza huku nikimshangaa. “Urafiki na wanaume, unatukera,” alisema mwanafunzi yule. “Kwani inakuhusu nini? Nikiwa na marafiki wa kiume si mimi, kwani wewe?” nilimuuliza, na mimi nilionekana kuanza kukasirika. “Utakuwa na matatizo tu, mwili wako haupo sawa kabisa,” aliniambia maneno ambayo yaliufanya moyo wangu kughadhabika.
AFAGILIA HESABU
Sikutaka kubadilika, urafiki na wanaume wala haukuisha, kila siku nilijiongezea marafiki wengi maishani mwangu. Darasa letu lilikuwa limegawanyika, kulikuwa na wanafunzi waliokuwa wapole mno, kulikuwa na wale ambao walikuwa wakorofi na hata wasichana ambao kila siku walijiona kuwa ni bora zaidi ya wengine.
Katika masomo yote tuliyokuwa tukifanya, niliyapenda zaidi masomo ya Hesabu na Historia. Masomo mengine yalinisumbua mno kwa mfano Kiingereza na Jiografia, kwa sababu yalitumia lugha kwa sana. Ila kwa hesabu, haikutakiwa ujue sana lugha, ilikuwa ni kucheza na namba tu. Kwa somo la Historia, kitu kilichokuwa kikinifurahisha ni kusikia stori za zamani ambazo kwangu zilionekana kunistaajabisha. Hata katika ufanyaji wa masomo yangu, masomo hayo mawili ndiyo niliyamudu zaidi.
Sikuwa mchoyo, kila nilichokuwa nikikifahamu, nilipenda wenzangu wakifahamu lakini si kila mwanafunzi alikuwa hivyo, wapo wengine ambao mara walipokuwa wakikifahamu kitu, hawakutaka wengine wakifahamu, walitaka kuwa nacho wao tu. Kwa miezi sita, nilikuwa nikihangaika kuifahamu lugha ya Kingereza tu.
Kazi kubwa kuifahamu lugha hiyo haikuwa kwangu tu bali hata kwa wanafunzi wengine ambapo mpaka wengine walikuwa wakishinda na Kamusi ya Kiingereza lakini hawakuambulia kitu. Wakati kila kitu kikiendelea, hapo sikuweza kukaa kimya, mishemishe zangu za kuanza kuimba zikaanza tena kama nilivyokuwa nikifanya kila nilipokwenda madrasa.
AANZA KUIMBA SEKONDARI
Nilipoanza kuimba hapo shuleni mbele ya wanafunzi wenzangu, nakumbuka kuna baadhi walinikejeli kwa kuniona sijui kuimba huku wengine wakisema kwamba sauti yangu haikuwa nzuri na ilisikika kama konokono.
Maneno hayo yaliniuma lakini sikuwa na jinsi, ili kufika pale nilipokuwa nikipahitaji nilitakiwa kudharauliwa sana na kusemwa na watu wangu wa karibu hivyo wakati mambo hayo yote yanatokea, sikutakiwa kukata tamaa zaidi ya kusonga mbele.
“Hilo lisauti lako, libaya kweli halafu unataka kuimba kama Bi. Kidude, utaweza?” aliniuliza mwanafunzi mmoja, alikuwa msichana, maneno yake yakanifanya kuona kwamba hata naye alikuwa na fitina. “Hakuna bwana usimkatishe tamaa, mbona anajua kuimba tu,” alisema mvulana mmoja, kidogo nikapata faraja upya. “Hajui kuimba, sauti lake libaya kweli mpaka masikio yangu yanauma,” alisema yule msichana