Hivi
karibuni kumezuka tabia za utapeli unaofanywa na wanaojisadikisha kuwa
ni watumishi wa Umma au Mawakala wa kusimamia uhamisho wa Watumishi
kuhama kutoka Mkoa mmoja kwenda Mkoa mwingine na pia kujihusisha na
kutoa taarifa za uongo kwa kugushi nembo za Ofisi ya Rais.
– TAMISEMI kuhusu ajira, kupandisha madaraja ya walimu.
Yamekuwepo Malalamiko mengi kutoka kwa
wahanga/waathirika wa tabia hiyo kwa nyakati tofauti ambayo watumishi
wamehadaiwa kuwa watasaidiwa kuhamia sehemu yoyote wanayoihitaji baada
ya kulipa kiwango cha fedha ambacho hupangwa na wahalifu hao. Miongoni
mwa taarifa batili wanazosambaza ni Uhamisho na Ajira za Walimu.
Matangazo hayo pia yameonekana katika
mbao za matangazo za baadhi ya Halmashauri. Mara nyingi watu hao huweka
namba zao za simu kwa ajili ya kupokea fedha za uhamisho kutoka kwa
watumishi pamoja na kuweka anuani za barua pepe zinazosadikiwa kutumika
katika kukusanya barua za maombi ya uhamisho.
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI) inapenda kuchukua fursa hii, kutoa
taarifa hii kwa lengo la kuujulisha Umma wa Watanzania juu ya kuwepo kwa
uhalifu huu ili waweze kujiepusha nao.
Ofisi ya Ras –TAMISEMI haitasita kuchukua hatua za Kisheria kwa wale wote watakaobainika kujihusisha na uhalifu wa aina hii.
Tunasisitiza kuwa wananchi wafuate
taratibu na pia watambue kuwa hakuna malipo yoyote yanayotakiwa ili
kuhamisha mtumishi. Wananchi wanaombwa kutoa taarifa pale watakapoona
kuna utapeli unaoendelea katika masuala ya ajira na uhamisho.
Watumishi wanaweza kufahamishwa juu ya
taratibu za uhamisho katika Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa,
Wakurugenzi wa Halmashauri na pia kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais
-TAMISEMI (www.tamisemi.go.tz).
Ofisi ya Rais TAMISEMI haijatoa matangazo yoyote yanayohusiana na Ajira za Ualimu katika kipindi hiki.
Imetolewa na:-
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
15 Septemba, 2016