Shirika hilo lilizichukua mali
mbalimbali za kampuni za Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai,
wiki iliyopita kupitia mawakala wa kampuni ya Fosters Auctioneers katika
jengo lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi
(Makunganya) jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ya NHC ilitokana na mgogoro
wa muda mrefu, wakimtuhumu Mbowe kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh.
1.3 bilioni, ikiwa jumla ya fedha za kodi ya kupangishwa kwenye jengo
hilo.
Kutokana na mvutano huo, Mbowe
alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, kupinga hatua ya
NHC kumuondoa katika jengo hilo, pamoja na kuchukua mali zake huku
wakitangaza kuzipiga mnada baada ya siku 14 tangu kuzichukua.
Jana, Jaji Siyovelwa Mwangasi alitoa
zuio na kuiamuru NHC kutouza wala kupiga mnada mali hizo za Mbowe mpaka
mahakama hiyo itakapotolea uamuzi katika kesi ya msingi.
Katika kesi hiyo namba 722 ya mwaka 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili Peter Kibatala na Omary Msemo.
Jaji Mwangasi amesema kuwa,
anakubaliana na maombi ya mlalamikaji na kutaka mali hizo zisiuzwe hadi
hapo mahakama itakapofanyia uamuzi kesi ya msingi.
Hatua hiyo inakuja baada ya upande wa
NHC kupitia mawakili wake Aloyce Sekule na Miriam Mungula kushindwa
kuwasilisha hoja za msingi kueleza, ni kwanini zuio hilo lisitolewe hadi
hapo kesi ya msingi itakapoanza kusikilizwa.
Awali, mawakili wa NHC, walidai kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya Mbowe kwa kuwa
hakuna kesi ya msingi ambayo imefunguliwa, hivyo maombi hayo yatupiliwe
mbali.
Wakili Kibatala alijibu hoja hiyo kwa
kusema, hatua ya kuwasilisha maombi hayo inalenga kubaini kama kweli
Mbowe anadaiwa kodi ama la.
Kibatala alidai kuwa mahakama hiyo ina
mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo inaweza ikatoa uamuzi wowote, na
ndiyo maana wamewasilisha maombi hayo ili itolewe amri ya muda ya
kuzuia mchakato huo.
Miongoni mwa hoja za Mbowe
alizoziwalisha mahakamani hapo, ni pamoja na hoja kuwa, yeye (Mbowe) na
shirika hilo walikubaliana kwamba atalikarabati na kulipanua jengo hilo
kwa asilimia 100. Makubaliano ambayo yaliingiwa mwaka 1997.
Amedai kuwa katika makubaliano hayo
yeye na NHC walikubaliana watamiliki jengo hilo kwa pamoja kwa muda wa
miaka 99, huku Mbowe katika mgawanyo wa mapato akitakiwa kupata asilimia
75 na NHC ikitakiwa kupata asilimia 25.
Pia alieleza kuwa katika makubaliano
hayo, licha ya mwenendo wa kibiashara kutokuwa mzuri, muda wote alikuwa
akilipa asilimia hiyo 25, kwa mujibu wa makubaliano yao.
Hivyo kutokana na hatua ya NHC kuvunja
mkataba huo kwa kumtoa kwenye jengo na kuchukua mali zake, anaiomba
mahakama iliamuru shirika hilo limlipe fidia.
Mbowe aliondolewa kwenye jengo husika mnamo Septemba mosi kwa madai ya kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. bilioni 1.3.
Mawakala wa NHC walifika katika jengo
hilo saa 12:30 asubuhi na wafanyakazi zaidi ya 50 na kwenda moja kwa
moja katika kampuni ya Free media pamoja na ukumbi wa Bilcanas na
kuchukua vifaa mbalimbali ikiwemo, meza, viti na kompyuta.
Siku chache baada ya kuondolewa kwa
Mbowe katika jengo hilo, Rais John Magufuli alilisifu shirika hilo kwa
hatua hiyo na kulitaka lichukue hatua kama hizo kwa wadaiwa wengine
zikiwemo taasisi za umma