Jeshi
la Polisi Wilaya ya Chakechake, Pemba limezuia kufanyika mkutano na
vyombo vya habari wa Chama Cha Wananchi (CUF) uliokuwa umepangwa
kufanyika leo wilayani humo, kupisha ziara ya Rais John Magufuli
itakayoanza leo.
Rais Magufuli anatarajia kuanza leo ziara yake ya kwanza visiwani humo tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Ikulu, Rais Magufuli atazulu Pemba leo na kesho atakuwa Unguja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini
Pemba, Shekhani Mohamed Shekhani amesema kuwa zuio hilo la mkutano wa
CUF ni kwa sababu eneo wanalotarajia kutumia liko jirani na eneo la
uwanja atakaokuwa akihutubia Rais Magufuli.
Hata hivyo, Katibu wa CUF wilaya ya
Chake Chake, Saleh Nassor Juma alilalamikia maamuzi hayo ya Jeshi la
Polisi kwa madai kuwa wao walitaka kufanya mkutano na vyombo vya habari
na sio mkutano wa hadhara. Alisema kuwa tayari walishawaeleza Idara ya
Habari Maelezo na waliridhia.
Alisema mkutano huo na waandishi wa
habari ulilenga katika kutoa tamko lao kuunga mkono uamuzi uliochukuliwa
na Baraza Kuu la chama hicho kumsimamisha uanachama aliyekuwa
Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na viongozi wengine 10.
“Niliwakatalia kwa hoja kwamba
mkutano na waandishi wa habari ni haki yetu ya kikatiba na
tulikwishawataarifu watu wa Idara ya Habari Maelezo juu ya kikao hicho
halali ambacho wao pamoja na waandishi wa habari walithibitisha kuwa
watahudhuria,” alisema Nassor.
Idara ya Habari Maelezo ilithibitisha
kuwa walikubali kufanyika kwa mkutano huo wa CUF na vyombo vya habari
lakini baadae walipokea taarifa ya kuahirisha kupisha ugeni wa Rais
Magufuli.