
WAZIRI
wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako ametoa siku saba kuanzia jana kwa vyuo vikuu nchini, ambavyo
vimepokea fedha za mikopo za wanafunzi ambao hawapo chuoni, kurejesha
fedha hizo.
Aidha,
amesitisha mikopo kwa wanafunzi wote 2,192 ambao walipuuzia kuhakikiwa
hata kama wapo wenye sifa hadi pale watakapojaza upya fomu za kuomba
mikopo, kwa kuwa wamekaidi agizo la serikali.
Profesa
Ndalichako alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake Dar es Salaam jana, akitoa taarifa ya kazi ya uhakiki wa wanafunzi
wanufaika wa mikopo kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini.
Alisema
katika uhakiki huo kwa mara ya kwanza wanafunzi 2,763 hawakujitokeza,
baada ya taarifa hiyo kutolewa kwenye vyombo vya habari na majina yao
kuwekwa hadharani, awamu ya pili na ya tatu walijitokeza wanafunzi 571
na kuhakikiwa.
“Uhakiki
wa malipo yaliyofanyika unaonesha kuwa wanafunzi hao 2,192 ambao
hawakujitokeza kuhakikiwa wameigharimu serikali kiasi cha Sh
3,857,754,460 kwa mwaka wa fedha 2015/2016,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema
uhakiki huo ulifanywa kwa vyuo vya elimu ya juu 31 kati ya 81 vilivyopo
nchini na kwamba kazi hiyo ilifanywa kwa awamu tatu mfululizo, baada ya
wizara kuunda timu ya kuhakiki wanafunzi kwenye taasisi za elimu ya juu
nchini ili kuiridhisha na uhalali wa wanafunzi wanaopata mikopo kwa
ajili ya elimu ya juu.
“Uhakiki
ulifanywa na watumishi wa Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kati ya mwezi Mei hadi Julai
mwaka huu. Wanafunzi wanufaika wa mikopo walitakiwa kujitokeza na
kuonana na timu ya uhakiki ana kwa ana ili kutambuliwa na kuhakikiwa,”
alieleza.
Baadhi
ya idadi ya wanafunzi wa chuo ambao hawakuhakikiwa na kiasi cha fedha
walicholipwa ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) idadi ya wanafunzi
wasiohakikiwa 350, fedha zilizolipwa kwa wasiohakikiwa Sh 703,438,635,
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wanafunzi 364, Sh 460,963,550, Chuo Kikuu
cha Mtakatifu Joseph Dar es Salaam wanafunzi 200, Sh 408,854,325, Chuo
Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), wanafunzi 235, Sh 387,625,650, Chuo
Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), wanafunzi 84 Sh 146,190, 775, Chuo
cha Usimamizi wa Fedha (IMF), wanafunzi 85, Sh 147,314,075 na Chuo
Kikuu cha Ushirika Moshi (MOCU), wanafunzi sita, Sh 14,160,000.
Profesa
Ndalichako alisema kutokana na mambo hayo yaliyobainika, pia serikali
imeviagiza vyuo vikuu kuwasilisha Bodi ya Mikopo kwa wakati taarifa zote
za kitaaluma na za kibenki za wanafunzi ili kuiwezesha Bodi ya Mikopo,
kufanya marekebisho stahiki katika kumbukumbu zao na kuepusha ulipaji wa
fedha kwa wanafunzi wasiostahili.
Aidha,
Bodi ya Mikopo imetakiwa kuchambua na kuingiza mara moja mabadiliko ya
taarifa za wanafunzi kama zilivyopokelewa kutoka vyuoni ili kuepusha
ulipaji wa fedha kwa wanafunzi wasiostahili. Alitaka kuchukuliwa kwa
hatua kali za kinidhamu kwa wote waliohusika kufanikisha malipo kwa
wanafunzi ambao hawapo vyuoni.
“Hii
inahusisha wafanyakazi wa bodi ya mikopo na vyuo husika,” alifafanua
huku akivitaka vyuo kuweka utaratibu mzuri wa kudhibiti malipo kwa
wanufaika wa mikopo ili kuepuka kufanya malipo kwa wanafunzi hewa. Mbali
na hilo, aliwataka wakuu wa vyuo kuweka mfumo wa kuhakiki usahihi na
matokeo ya wanafunzi yanayotumwa na Bodi ya Mikopo na watawajibika kwa
usahihi wa taarifa zinazowasilishwa. “Kwani zoezi la uhakiki limebaini
kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye matokeo ya wanafunzi, wapo ambao
hawakufanya mtihani au waliofeli lakini wameandikiwa ‘pass’ ili
waendelee kupata mikopo,” alisema.
Alisisitiza
uchunguzi zaidi kufanyika kwa miaka iliyopita ili kubaini fedha za
mikopo zilizolipwa kwa watu wasiostahili, akisema hatua hiyo inatokana
na matokeo ya uchunguzi kubaini kuwa wapo baadhi ya wanafunzi
waliohitimu tangu mwaka 2013, lakini wameendelea kupokea fedha na
wengine waliofukuzwa kwa kushindwa masomo tangu mwaka 2013/2014 lakini
bado wamelipwa hadi mwaka 2015/2016