
Waandishi
wa habari kutoka China wakiongozwa na balozi Liu Guzjin (wa tano
kushoto aliyenyoosha mkono) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi
wa TANAPA Bw. Allan Kijazi (wa tano kushoto walio simama), Afisa
Uhusiano Mkuu wa TTB Bw. Geofrey Tengeneza (wa tano kulia waliosimama)
na maafisa wa hifadhi ya Mikumi muda mfupi baada ya waandishi hao kutoka
China kuwasili katika hifadhi ya Mikumi.

Mkurugenzi
Mkuu wa TANAPA Bw. Allan Kijazi akizungumza na waandishi wa habari wa
China katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi mara baada ya kutembelea hifadhi
hiyo..
Afisa
Uhusiano Mkuu wa TTB Bw. Geofrey Tengeneza akizungumza na mkuu wa
msafara wa waandishi wa habari kutoka China balozi Liu Guzjin muda mfupi
kabla balozi huyo hajakabidhiwa DVDs na machapisho ya TTB yanayoelezea
vivutio vya utalii wa Tanzania.
Waandishi
wa habari 17 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini China ikiwemo
cctv wakiongozwa na balozi Liu Guzjin wapo hapa nchini kwa ziara ya siku
nne ambapo jana walitembelea hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kuvutiwa na
wanyama wa aina mbalimbali wakiwemo tembo, simba, makundi ya nyati na
wengineo wanaopatikana katika hifadhi hiyo.
Aidha
waandishi hao wa habari walivutiwa pia na ukarimu wa watanzania kwa
ujumla na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania kama eneo
bora la Utalii barani Afrika kwa wananchi wa China kupitia katika vyombo
vyao vya habri wanavyofanyia kazi.
“Tumefurahishwa
kuona wanyama wa kuvutia miongoni mwao wakiwemo wale maarufu watano
lakini pia na ukarimu wa watu wa Tanzania, na kwa kweli watanzania ni
rafiki zetu. Tunaahidi takuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania kwa
ndugu zetu nchini China.” Alisema Balozi Liu. Ameongeza kuwa Tanzania
ni nchi yenye vivutio vizuri vya utalii ambavyo hapana shaka kabisa
wachina wengi watapenda kuja kuvitembelea na kuviona.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) Bw.
Allan Kijazi aliwaambia wandishi hao muda mfupi baada ya waandishi hao
kutembelea hifadhi hiyo kuwa Shirika lake limejipanga vema katika
kuimarisha uhifadhi wa wanyama na vivutio vingine vya utalii vilivyo
ndani ya hifadhi zote za Taifa pamoja na mazingira yake kwa lengo la
kuhakikisha kuwa utalii unakuwa endelevu.
Naye
AfisaUuhusiano Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Bw. Geofrey
Tengeneza akizungumza ujio wa waandishi hawa kutoka China utasaidia
katika kuitangaza sana Tanzania kama eneo la utalii kwa watu wa China na
hasa ikizingatiwa kuwa soko la China ni miongoni mwa masoko
yanayolengwa sana na TTB kupitia mpango wake mkakati wa utangazaji
utalii Kimataifa.
Pamoja
na mambo mengine waandishi hao walitarajiwa pia jana kutembelea kituo
cha Kilimo kinachoendeshwa na China kilichoko Morogoro na kutoa msaada
wa vifaa vya kilimo. Aidha leo waandishi hao wanatarajia kushiriki
katika mkutano wa Kimataifa baina ya China na Afrika kujadili maendeleo
ya kidiplomasia utakaofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa
Julius Nyerere uliopo jijini Dar es salaam.
