
Na: Lilian Lundo na Sheila Simba - MAELEZO
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ametoa
siku saba kuanzia Agosti 17, 2016 kwa vyuo vikuu kurejesha fedha
zilizopokea ambazo ni za wanafunzi ambao hawapo chuoni.
Prof.
Ndalichako ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea
na waandishi wa habari juu ya taarifa la zoezi la uhakiki wa wanafunzi
wanufaika wa mikopo vyuo vya Elimu juu.
Prof.
Ndalichako amesema kuwa uhakiki wa wanafunzi hao umefanyika katika
vyuo 31 kati ya vyuo 81 vilivyopo nchini, Katika utafiti huo wanafunzi
2,192 wameshindwa kuhakiki majina yao, hivyo kushindwa kuthibitisha
uwepo na uhalali wa wanafunzi hao.
“Mikopo
ya Wanafunzi hao imesitishwa na kwa wale ambao ni wanafunzi halali
lakini walishindwa kujihakiki itabidi waombe tena mkopo,” alifafanua
Mhe. Ndalichako.
Ameendelea
kwa kusema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2015/16 wanafunzi hao hewa
wameigharimu Serikali kiasi cha shilingi 3,857,754,460, kiasi ambacho
kinatakiwa kurejeshwa na vyuo ambavyo wanafunzi hao wamebainika.
Aidha,
Prof. Ndalichako amesema kuwa taarifa hiyo imekabidhiwa kwenye vyombo
vya sheria ili kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya
udanganyifu na kusababisha Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
Vile vile Prof. Ndalichako amewataka wakuu wa vyuo kuweka mfumo wa kuhakiki usahihi wa matokeo ya wanafunzi yanayotumwa Bodi ya Mikopo kutokana na vyuo vingi kubainika kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye matokeo ya wanafunzi ambao hawakufanya mtihani au waliofeli na kuandikiwa wamefaulu ili waendelee kupata mikopo.