
SIKU
mbili baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuahidi kufanyika maridhiano
kati ya uongozi wa Bunge na wabunge wa upinzani katika kikao kijacho
kinachotarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu, Naibu Spika, Dk. Tulia
Ackson amesema hataki kuwasikia wabunge wa upinzani wala kuwawaza.
Kauli hiyo ya Naibu Spika huenda
ikazidi kutonesha kidonda hasa baada ya Bunge la Bajeti lililofanyika
Mei mwaka huu kuacha majeraha kutokana na wabunge wa upinzani wanaounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vyote vilivyoendeshwa
na kiongozi huyo.
Juzi wakati akihojiwa kupitia
kipindi cha Funguka kinachorushwa na Kituo cha Luninga cha Azam, Spika
Ndugai, alisema anatafuta mbinu ya kuweka sawa mambo hayo kwa kufanya
maridhiano ikiwemo kushirisha maspika wastaafu.
Akizungumza na gazeti la Mtanzania
juzi katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Dk.
Tulia alisema hapendi kuwawazia wabunge hao wa upinzani.
“Kwa kuwa Spika yeye kazungumza siwezi kucomment chochote kwa sababu sipendi kuwawazia wabunge hao,”alisema.
Alipoulizwa kwamba ni kwanini
migogoro ilizidi wakati yeye akiwa anaendesha vikao, alisema alichokuwa
anafuata ni kanuni na kwamba malalamiko hayawezi kukosekana.
“Nashangaa wengine wanasema
kuendesha vikao ni mpaka uwe na uzoefu…unajua zile kanuni hata ukipewa
uendeshe wewe ukishazielewa hazihitaji uzoefu wowote. Kulalamika kuwa
nawapendelea ni jambo la kawaida.
“Kwa mfano siku iliyotokea vurugu
wakati wabunge wa upinzani wanadai kutorushwa matangazo ya Bunge live,
aliyekuwepo kwenye kiti alikuwa ni mwenyekiti ambaye ni mzoefu wa siku
nyingi na ni yeye aliyepeleka majina yao kwenye Kamati ya Maadili, sasa
sidhani kama hiyo ni hoja,”alisema Dk. Tulia
Alieleza kushangazwa kwa kitendo
cha wabunge wa upinzani katika barua yao waliyomwandikia Spika kwamba
hawana imani naye, huku akihusishwa na fedha zilizorejeshwa serikalini.
“Katika ile barua walieleza sababu nyingine kuwa hawana imani na mimi, wakanihusisha na zile Shilingi bilioni 6 zilizorejeshwa serikalini wakati sheria na utaratibu upo wazi kwa sababu Spika au Naibu Spika hauhisiki na masuala ya fedha bali anayehusika ni Katibu wa Bunge.
“Kwa
hiyo ni jambo la kushangaza kwamba Naibu Spika karudisha fedha, mimi si
mshika mafungu lakini pia ni namna watu walivyopokea huwezi kuwazuia
wanavyokuwazia,” alisema.
Akizungumzia kauli ya Spika Ndugai
kwamba kwa kuwa Bunge la 11 lina wabunge wapya wengi na kwamba
kuwaongoza kunahitaji uvumilivu mkubwa alisema: “Nisingependa kuongelea
kauli ya Spika…lakini uvumilivu wa mtu kutakiwa akae hadi mara 11 halafu
ameendelea kusimama ni uvumilivu gani huo?,” alihoji.
Pamoja na mambo mengine alisema
wakati wabunge wanawake wa Ukawa walipojitoa kwenye Chama cha Wabunge
Wanawake (TWPG), alitukanwa tusi kubwa lakini alinyamaza.
Mei 5, mwaka huu wakati akichangia
mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya
Katiba na Sheria, Mbunge wa Ulanga Mashariki, Gudluck Mlinga (CCM),
alidai kuwa ili kuwa mbunge wa viti maalumu Chadema lazima uwe ‘baby’ wa
mtu.
“Laiti ungeona Hansard tusi walilonitukana siku ile, actually Mlinga hajatukana lakini ulisikia nikilalamika mahali kwamba nimetukanwa? wao wanaongee vibaya…watukane, mimi bado ni kiongozi wao na siwezi kuanza kuwakasirikia itakuwa sasa nashindwa kuwaongoza mimi ni kama mzazi wao,” alisema Dk. Tulia.
Alisema
kitendo cha watu kudai kwamba anafanya upendeleo bungeni ni changamoto
ya kawaida, kwa sababu hata katika mabunge ya Jumuiya ya Madola
malalamiko ya aina hiyo yapo.
“Pale bungeni wako wabunge 389, hawa ni wengi sana wote hawawezi kupata nafasi ya kuongea. Kwa mfano uliomba nafasi jana ukapewa ukaomba leo, hata ukisimama mara 11 katika hali ya kawaida huwezi kupewa kwa sababu wako wengi ambao hawajachangia.
“Kama
kiongozi naona ni sehemu mojawapo ya kusimamia jamii ni changamoto na
itaendelea kuwepo kwa miaka mitano,”alisema Dk. Tulia.
chanzo bofya HAPA