“SIZONJE namjua unataka
nikwambie? Nitakwambia. Kuna sehemu uliimba vile vyumba vitatu
visivyofunguka milango, sasa mimi nitakuonyesha funguo zake zilipo,”
hayo ni maneno ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe
Magufuli akimwambia mkali wa mashairi ya kughani, Mrisho Mpoto.
Kauli hiyo, ilikuja mara baada ya
kushuka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar
alipokuwa akitokea Mwanza, ambapo alipokelewa na kikundi cha ngoma cha
Mpoto na ndipo Magufuli alipopata nafasi ya kuzungumza kwa ufupi na
msanii huyo.
Hiyo ni bahati ya kipekee kwa msanii kuzungumza na rais wa nchi na kupewa ujumbe huo.
Wimbo wa Sizonje umejaa mafumbo mengi
kuanzia jina la wimbo hadi mashairi yake, inahitajika akili ya ziada
kudadavua yale yanayoimbwa na Mpoto.
Binafsi nimekuchambulia baadhi ya mashairi ya wimbo huo ambao unapendwa na Rais Magufuli:
Sizonje hii ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Sizonje ndio nyumba yetu
Milango ipo wanapita madirishani
Ingia uyaone, maajabu ya nyumba yetu
Ingia uyaone, maajabu ya nyumba yetu
(Mpoto anamueleza Sizonje
kama ndiyo rais aangalie nchi yetu na apambane na wale wanaopita njia za
panya kupata mafanikio wakati njia halali zipo)
Karibu sana Sizonje, hii ndo nyumba yetu
Tulipoficha mundu za kupondea wezi
Kwani, makaburi yaliofukuliwa lazima yazikwe upya?
Nyumba hii Sizonje ina vyumba vinne
Vitatu havifunguki, kimoja hakina mlango
Japokuwa kina watu ndani, na hawaongei Kiswahili
Wenyeji wanalala sebleni na walishazoea.
Sizonje kule tulipotoka panaitwa jikoni
Huna haja ya kwenda kule, kumejaa mafundi wa kupika
Sasa hivi wanakupikia wewe ili ule ulale
Ukiamka muongee nini hasa ujio na dhima ya safari yako
Wanashangaa mbona ghafla
Samahani sana mgeni
Wapishi wameniomba kwamba
Nikuulize tena kwa kukuomba kwamba
Eti unapenda vya mafuta au vya nazi?
Wanataka kukuonyesha madoido katika mapishi yao Sizonje
(Rais anaoneshwa wizara nyeti zilizopo ndani ya nchi, wapishi
ni viongozi wanaoongoza wizara hizo ambao wao ndiyo wanajifanya wanajua
mipango yote, wanakukaribisha kama unatka kuingia kwenye mfumo wao).
Sizonje chumba hiki naomba usiingie
Ukimaliza nitakwambia kwa nini
Kuna sauti inajirudia mara kwa mara
Na hapa mlangoni kulikuwa na picha mbili kubwa
Moja picha, nyingine mchoro wa picha wa kwanza
Ninachokumbuka iliwahi kuandikwa
“USIYEMTAKA KAJA”
Hatukuwahi kuelewa maana yake
Labda kwa sababu ya ujio wako unaweza kutusaidia
(Kuna watu ambao huwa
hawaguswi kwa kuwa wao
ndiyo wanaoshikilia mifumo, hivyo rais akitaka matatizo basi awaguse
watu hao kwa ubaya, usiyemtaka kaja hapa anamaanisha wapo waliokuwa
hawapendi awe rais lakini amekuwa).
[VESI 2 – MRISHO MPOTO]
Najua, wimbo mbaya haufai kubembelezea mtoto
Na kamwe mtoto hawezi kuungua
Kwa kiazi kilichokuwa kwenye kiganja cha mama yake mzazi
Njoo huku uone Sizonje
Si unajua, harufu ya uzazi haiishi mpaka mtoto akue?
(Anamaanisha rais hawezi kumaliza ufisadi na uzandiki kwa mara moja kwa kuwa hayo ndiyo maisha ya watu kadhaa)
Sawa, Sizonje, huu hapa ni ua
Lile pale ni shimo la taka
Na kile pale ni choo
Kinachotutisha na kutuogopesha zaidi
Wanaoishi humu ndani
hawajawahi kutupa taka
Wala kwenda chooni
Kama ukiwa makini
Kwa nje utasikia sauti za makundi ya watu
Wengi ni vijana, wana bahasha za khaki mikononi
“KAMA HAMTUPI TAKA SHIMO HILI MLICHIMBA LA NINI?”
Lakini pia kwenye sauti zao, Sizonje
Kuna watoto, wazee na kina mama
Ukiunganisha sauti zao ndio unapata hizo kelele
Ninavyosikia, ila sina uhakika
Waliambiwa kihistoria nyumba hii ni ya kwao
Na wana haki ya kutupa taka na kutumia choo hiki
Sasa, njoo nikuonyeshe huku uchochoroni
Uone maajabu mengine ya nyumba hii
Sizonje, ukiona tembo anaringa
Ujue mvua zinakaribia
(Taka imetumika kama soko la
ajira kwamba wenyeji hawapati ajira na ajira nyingi zimekuwa za
kujuana. bahasha maana yake ni vyeti. Anauliza kama wanasoma ajira
hawapati kwa nini walienda shule?)