Ingawa haikufahamika sababu ya kuondolewa kwake, huenda mvutano baina yake na Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa ukawa umechangia.
Saa 2:12 asubuhi jana, Ofisi ya Waziri
Mkuu ilikuwa imeshatoa taarifa kuwa uteuzi wa Ntibenda umetenguliwa na
nafasi yake imechukuliwa na Mrisho Gambo ambaye aliteuliwa hivi karibuni
kuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu haikueleza sababu za kutenguliwa uteuzi wa Ntibenda ambaye amekuwa Arusha tangu mwaka 2014.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ntibenda,
ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu kabla ya kuteuliwa kushika
wadhifa huo mwaka 2014, amehamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu ambako
atapangiwa kazi nyingine.
Jana, Ntibenda alikuwa akisubiriwa
kufungua mkutano wa shirika la kimataifa la afya kwa vijana (AMREF) na
tayari tangu asubuhi alikuwa ofisini kwake kujiandaa kwa majukumu hayo
ya siku.
Mbali na mkutano huo, Ntibenda
alitarajiwa kushiriki kama mwenyeji katika mkutano wa Mfuko wa Maendeleo
(Tasaf) ambao ulishirikisha wakuu wote wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini
pamoja na wakuu wa wilaya.
Kwenye mkutano wa AMREF, Ntibenda
alisubiriwa kwa muda mrefu hadi habari za kutenguliwa kwa uteuzi wake
ziliposambaa, ndipo akateuliwa mganga mkuu wa mkoa, Frida Mokiti
kufungua mkutano huo.
Habari za uhakika kutoka ofisi ya mkuu
wa mkoa zinasema kuwa kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutenguliwa
kwake, Ntibenda alikuwa na mazungumzo na Gambo ofisini kwake.
Haikujulikana mara moja mambo
waliyozungumza wawili hao, ingawa tangu Ntibenda ateuliwe kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Arusha kumekuwa na utulivu wa kisiasa.
Ntibenda alikuwa kwenye mzozo na
viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambao walikuwa
wakimlalamikia kuingilia majukumu ya jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa, Lengai
ole Sabaya aliwaambia waandishi wa habari mapema wiki iliyopita wakati
akisoma maazimo ya kamati ya utekelezaji, kuwa mkuu huyo anakwamisha
utendaji wao.
Katika taarifa hiyo UVCCM ilisema
kitendo cha Ntibenda kuingilia kati sakata la mikataba ya wapangaji
katika maduka ya jumuiya hiyo ni kuwakwamisha.
Baadaye kundi la viongozi hao wa UVCCM
pia lilidaiwa kuandika barua ya kumlalamikia Ntibenda kutokana na
kutoridhishwa na utendaji wake.
Hata hivyo, Ntibenda alikanusha tuhuma
zote za UVCCM kumtetea mmoja wa wapangaji na kusema anasikitishwa na
madai hayo dhidi yake.
Uteuzi wa Gambo
Wakati Ntibenda akienguliwa, baadhi ya viongozi wa UVCCM jana walikuwa wenye furaha baada ya Gambo kupandishwa cheo.
Mbunge wa viti maalumu, Catherine Magige alimpongeza Rais Magufuli kwa uteuzi wa Gambo ambaye alisema ni zao la jumuiya hiyo.
Magige alisema uteuzi huo unaonyesha jinsi gani Rais Magufuli alivyo na imani na vijana na akawataka kuendelea kumuunga mkono.
“Tunaamini Gambo ataleta mabadiliko makubwa ya utendaji katika Mkoa wa Arusha kwa kuwa ni mchapakazi,” alisema.
Wakati Magige akisema hayo, Ole Sabaya alisema Rais Magufuli amesikia kilio chao.
“UVCCM tulikuwa na malalamiko juu ya utendaji wa mkuu wa mkoa, sasa tunashukuru sana Rais Magufuli kusikiliza kilio chetu,” alisema Ole Sabaya.
Kuondolewa Ntibenda
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa mbunge
wa Arusha, Godbless Lema aliyesema anaona vurugu zikirudi na kwamba
uteuzi wa Gambo ni kama mkakati wa kuhakikisha wapinzani
wanasambaratishwa mkoani Arusha ambako ni moja ya ngome za Chadema.
Lema, ambaye amekuwa katika mgogoro na
Gambo katika siku za karibuni, alisema kada huyo ameteuliwa ili
kuidhibiti Chadema, jambo ambalo chama hicho hakitakubali.
“Hivi karibuni nilimwambia mkuu wa
mkoa Ntibenda kuna watu wanakutafuta, sasa wamefanikiwa. Lakini mimi
naona Arusha ijayo itakuwa na vurugu tofauti na utulivu uliopo sasa,” alisema.
Hata hivyo, alisema Chadema imejipanga kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na kamwe haitakubali kuhujumiwa na mtu yeyote yule.
Alipotafutwa jana asubuhi, Gambo alisema hana cha kuzungumza na kwamba hakuwa na taarifa rasmi.
Gambo, ambaye jana alishiriki mkutano
wa Tasaf kwa nafasi yake ya mkuu wa Wilaya ya Arusha na baadaye
kuondoka, alisema alikuwa hajapata taarifa rasmi.
Hata hivyo, akiwa kwenye mkutano
baadhi ya wakuu wa mkoa na wakuu wa wilaya za mikoa ya Kanda ya
Kaskazini, walimpongeza kwa uteuzi huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,
Richard Kwitega alisema alipata taarifa za uteuzi huo jana asubuhi na
alipata maelekezo kuwa Gambo anatakiwa Dar es Salaam.
“Nilipata taarifa rasmi ya uteuzi wake na tayari tulikuwa naye hapa ofisini ili kuweka taratibu za kwenda kuapishwa,” alisema.
Alisema Gambo atarejea Jumamosi na
atapokewa na wafanyakazi na baadaye kushiriki mapokezi ya Mwenge wa
Uhuru wilayani Ngorongoro.
Chnzo: Nipashe