Mwenyekiti wa Chama cha UDP
John Cheyo amewataka Watanzania kupaza sauti na kukataa maandamano ya
Septemba Mosi mwaka huu ambayo yameandaliwa na Chama cha Demokrasia
(CHADEMA).
Cheyo ameyasema hayo leo jijini Dar es
Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake
juu ya maandamano hayo.
“Watanzania wenzangu jambo la
kuwaacha watoto wetu kwenda kupambana na Polisi si jambo zuri, wote
tupaze sauti zetu na kusema hapana kwa maandamano ya Septemba Mosi,” alisisitiza Cheyo.
Alisema kuwa, ziko njia mbalimbali
ambazo Chadema wanaweza kuzitumia kutatua migogoro, kama vile meza ya
mazungumzo na kuachana na maandamano ambayo yanachochea vurugu na hata
kutishia amani ya nchi.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi
linapotoa katazo la maandamano ni lazima utii uwepo, kwani Polisi wapo
kwa mujibu wa Sheria na Katiba. Ikiwa Chama hicho hakikuridhika na
katazo hilo basi wanatakiwa kuonana na Waziri anayehusika na Jeshi la
Polisi.
Akifafanua zaidi alisema kuwa Rais
Magufuli amekuwa akichukua hatua za makusudi za kutatua matatizo
mbalimbali kama vile kupambana na ufisadi, ambapo viongozi wengi wa
Serikali wamesimamishwa kazi au kufukuzwa kutokana na kujihusisha na
masuala ya rushwa.
Mwenyekiti huyo wa UDP amewataka
watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Magufuli ili aweze kutimiza ndoto
zake na yale ambayo ameyaahidi kwa ajili ya nchi ya Tanzania.
Aidha Cheyo aliwasifu viongozi wa Dini
ambao walikaa na Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na
kukubali kurudi bungeni bila pingamizi lolote.
Amewataka viongozi hao wa dini
kuendelea kuzungumzia suala la amani kwa Watanzania na Viongozi wa kiasa
ili kudumisha amani ya nchi