MARA: Mtoto mwenye ulemavu wa
ngozi (albino), Maria Maiya Marwa (15) wa Kijiji cha Kemakorere, Kata
ya Nyarero wilayani Tarime, Mara, amelia na kumuomba Rais Dk. John
Magufuli ‘JPM’ kumsaidia gharama za kumuwezesha kutibiwa saratani ya
ngozi nchini India baada ya kushindakana hapa nchini.
Akizungumza na gazeti hili akiwa
nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Albinism wa Wilaya,
Joseph Sinda mjini Tarime alipofikia kwa muda alisema alishindwa
kufanikiwa kupona hali yake hiyo licha ya kufikishwa katika Hospitali za
Muhimbili na Ocean Road zilizopo jijini Dar es Salaam alisema:
Maria Maiya Marwa
“Ninamuomba rais wangu Magufuli
anisaidie gharama za kuniwezesha kutibiwa tatizo langu hili la kansa ya
ngozi India kwani wazazi wangu hawana uwezo maana ni maskini,’’ alisema
Maria huku akibubujikwa na machozi.
Binti huyo alisema kuwa kabla ya
kufikishwa katika hospitali hizo, awali alipatiwa matibabu yake hayo
Hospitali ya Wilaya ya Tarime na ile ya Rufaa ya Musoma kwa nyakati
tofauti.
‘’Taarifa kwamba tatizo langu ni kansa
ya ngozi lilifahamika kutoka kwa madaktari wa Hospitali za Ocean Road na
Muhimbili, ambapo nilianza kutibiwa Juni 9, mwaka huu baada ya
kufikishwa hapo Januari 27, 2016,’’ alisema Maria huku akifuta machozi.
Alisema kuwa awali alikuwa akipatiwa
matibabu ya kawaida na kwamba Julai 26, mwaka huu aliruhusiwa kurejea
nyumbani kwao na madaktari wa Hospitali ya Ocean Road na kutakiwa
kurejea kuendelea na matibabu tena hospitali hapo Novemba 7, mwaka huu.
‘’Hapa mnapopaona nilipofungwa bandeji
pana kidonda kilichokula sikio langu la upande wa kulia na kinauma sana,
shingoni kuna sehemu imevimba, niliambiwa kuwa ni kansa ya ngozi,
niliambiwa na madaktari hao kuwa nirudi kuendelea na matibabu tena baada
ya miezi mitatu yaani tangu Julai 26, hadi Novemba 7, mwaka huu,
sidhani kama muda huo utafika kama sitasaidiwa na rais kwani ninateseka
mno maana sili vizuri kutokana na maumivu,’’ alisema Maria.
Kwa upande wake baba yake mzazi, Maiya
Marwa ambaye aliangua kilio akijutia uhali duni alionao na familia yake
hiyo, alisema hana jinsi ya kumuokoa kwa matibabu kwani hana kipato na
kuwaomba watu wenye uwezo wamsaidie mwanae huyo ili akatibiwe nchini
India.
Kwa walioguswa na mateso ya Maria watume misaada yao kwa simu namba 0766 128 337CHANZO: BOFYA HAPA