
POLISI mkoani
Kilimanjaro inawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kumuua kwa
kukusudia mwanamke Neema Ndewera (65), kwa kumchoma kisu shingoni na
sikio la kulia.Akitoa
taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod
Mutafungwa, watuhumiwa hao walifanya tukio hilo la kinyama Julai 10,
mwaka huu ambapo baada ya tukio hilo walifukia mwili wa marehemu kwenye
shimo la choo cha nje ya nyumba yake.
Alisema Ndewera alikuwa
akiishi peke yake katika kata ya Mbokomu, ambako Juni mwaka huu aliaga
anasafiri kwenda Arusha kuwaona watoto wake, ambapo alimuomba jirani
yake Michael John kuwa mwangalizi wa mifugo yake ambayo ni mbuzi wawili,
ng’ombe mmoja na kuku.
Alisema mwanzoni mwa
Julai, alirudi nyumbani kwake na kukuta mbuzi na kuku wameuzwa, hali
iliyomlazimu kumuuliza John kuhusu suala hilo ambalo hakupewa majibu ya
kuridhisha.
Mutafungwa alisema
kutokana na hali hiyo Julai 10, John akishirikiana na watuhumiwa
wenzake, wote kwa pamoja walimuua Ndewera ili asiwashtaki kwa wizi wa
mifugo.
Alisema baada ya tukio
hilo watuhumiwa hao waliuza ng’ombe aliyebaki kwa Sh 400,000 kisha
kugawana fedha, ambapo walidanganya kuwa Ndewera anaumwa na amesafiri
kwenda Dar es Salaam kwa mtoto wake kwa matibabu.
Alisema Agosti 12,
Polisi ilipata taarifa hizo kutoka kwa raia wema, ambapo walifika eneo
la tukio na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa kwenye shimo la
choo ukiwa na kisu shingoni, ambapo uchunguzi ulifanywa na madaktari na
kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu.
Kamanda aliwataja
watuhumiwa wa tukio hilo ni John (24) fundi ujenzi, Nevance Reginald
(46), Mussa Issa (23), Fausta Naftari (29) na Magreth John (53), wote
wanne wakijishughulisha na kilimo.