Jijini Mwanza Rais Magufuli
alipokelewa na maelfu ya wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake
tangu alipoingia kupitia kivuko cha Busisi – Kigongo na baadaye kupita
Usagara, Buhongwa, Mkolani, Nyegezi, Mkuyuni na Igogo ambako pamoja na
kuwahakikishia kuwa Serikali yake imejipanga kukabiliana na kero
mbalimbali za wananchi na kuwaletea maendeleo, amesitisha agizo la Jiji
la Mwanza la kuwataka wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la
Machinga kutofanya biashara zao katikati ya Jiji ifikapo tarehe 20
Agosti, 2016.
Pamoja na kusitisha agizo hilo, Dkt.
Magufuli amewaagiza viongozi wa Jiji la Mwanza na Halmashauri ya
Manispaa ya Ilemela kutafuta na kuandaa maeneo ambayo wafanyabiashara
hao watayatumia kwa ajili ya kufanyia biashara zao.
“Na mtakapowatafutia maeneo ya
biashara wapelekeni sehemu ambazo ni nzuri, msiwapeleke sehemu ambazo
hazina biashara, hawa wamachinga wanaendesha maisha yao kwa kutumia
biashara hizi” Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewahakikishia
wananchi wa Mwanza kuwa Serikali imeanza kufanya usanifu na upembuzi
yakinifu ikiwa ni maandalizi ya kuanza ujenzi wa daraja kubwa
litakalounganisha eneo la Busisi Wilayani Sengerema na Kigongo Wilayani
Misungwi ili kuondoa adha ya wananchi kuvuka eneo hilo kwa kutegemea
vivuko, na pia itahakikisha inanunua meli moja katika ziwa viktoria kama
ilivyoahidi.
Kabla ya kuingia Jijini Mwanza Rais
Magufuli alihutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Sengerema na pia
alizungumza na wananchi wa Sima Wilayani Sengerema na Kasamwa Wilayani
Geita ambako aliwahakikishia kuwa Serikali yake itaongeza msukumo katika
kutatua tatizo la uhaba wa maji katika maeneo hayo kwa kusambaza maji
ya kutoka ziwa Viktoria huku akiwataka viongozi halmashauri husika
kutumia rasilimali za halmashauri kutatua tatizo hilo la maji katika
maeneo ambayo hayatapitiwa na mradi mkubwa wa maji ya kutoka ziwa
Viktoria.
Katika hatua nyingine Mhe. Rais
Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa ya Mwanza na Geita kutafakari
sababu zilizosababisha kufa kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha NYANZA na
viwanda vya kuchambua pamba (Ginneries) ili kupanga namna ya kuvifufua.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo
alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kasamwa kilichopo
Wilayani Geita na ameahidi kuwa Serikali yake ipo tayari kuunga mkono
juhudi za wakulima kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao
yao ikiwemo zao la pamba.
Rais Magufuli atakamilisha ziara yake
ya siku mbili leo tarehe 11 Agosti, 2016 kwa kuweka jiwe la msingi
katika Daraja la watembea kwa miguu na kuzungumza na wananchi wa Mwanza
katika Uwanja wa Furahisha.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Mwanza
10 Agosti, 2016