Wakati Polisi ikimshikilia kwa
saa mbili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mkoani Mwanza, jeshi
hilo limefuta kongamano la kujadili Bajeti ya Serikali lililoandaliwa na
ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam huku kiongozi wake, Zitto Kabwe
akisakwa.
Jeshi hilo lilizuia mkutano wa hadhara
wa Chadema uliokuwa ufanyike wiki iliyopita mjini Kahama ambako
lilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanachama na wafuasi wa chama
hicho, katika kile kilichoelezwa kulikuwa na dalili za uvunjifu wa
amani.
Jeshi hilo pia lilizuia msafara wa viongozi wa chama hicho kuingia katika ofisi zake za Shinyanga walipokuwa wakielekea Mwanza.
Taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa
chama hicho, Tumaini Makene ilieleza kuwa mbali na Mbowe, jeshi hilo
pia lilikuwa linawashikilia Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema
(Bavicha), Patrobas Katambi na Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita.
Wengine ni Mbunge wa Tunduma, Frank
Mwakajoka na viongozi wengine na wanachama wa chama hicho waliokuwa
wanashikiliwa katika kituo cha Polisi Nyakato, jijini Mwanza.
Makene alisema tangu asubuhi ya jana,
Mbowe na viongozi wenzake walikuwa wakizunguka katika maeneo kadhaa ya
jijini Mwanza kuwasalimia wananchi katika ‘vijiwe’ mbalimbali kabla
hawajakamatwa.
Alisema, “Hadi sasa (saa 11 jioni) hakuna maelezo ya kushikiliwa kwao.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Ahmed Msangi alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao na kubainisha kuwa
waliachiwa bila kufunguliwa kesi yoyote.
“Walikutwa Igoma Sokoni
wakizungumza na wananchi. Mikutano ya namna hii imezuiwa. Wamefungua
kesi mahakamani, hivyo hakuna haja ya kufanya tofauti mpaka
itakapohukumiwa,” alisema Msangi.
Alifafanua kuwa jeshi hilo halina uhasama wowote na Chadema au chama kingine chochote na “hatuwezi kukiingilia kinapofanya mikutano yake ya ndani au hotelini. Kilichozuiwa ni mikutano ya hadhara.”
Wakati Msangi akisema hayo, kongamano
la ACT Wazalendo ambalo lilitakiwa lifanyike jana kuanzia saa 7:00
mchana kwenye Ukumbi wa Jengo la LAPF; Millennium Towers, Kijitonyama
lilizuiwa na polisi.
Tangu mapema asubuhi, askari polisi walitanda katika eneo la ukumbi huo kuzuia kongomano hilo.
Ukumbini hapo, waandaaji walisema
hakuna anayeruhusiwa kuingia kwani wamepewa maelezo ya kuufunga baada ya
tukio lililoandaliwa kuahirishwa.
Zaidi ya viti 210 vilikuwa vimepangwa
kwa ajili ya kongamano hilo na mmoja wa viongozi wa ukumbi huo
alionekana akiondoa mabango yaliyokuwa yanautambulisha mkutano huo wa
ACT.
Viongozi watatu wa ukumbi huo
walikataa kueleza kinagaubaga juu ya sakata hilo, lakini taarifa za
jumla zilisema mkutano umezuiwa.
Mmoja wa watumishi wa ukumbi huo, alisema: “Tuliandaa kila kitu, ila shughuli imeahirishwa. Ukumbi unatakiwa kufungwa. Hautatumika kwa leo.”
Ilipofika saa 5:00 asubuhi, Msemaji wa
ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis alisema chama kinafanya mkutano wa
dharura kwenye ofisi zake za makao makuu na baadaye kingezungumza na
waandishi wa habari.
Saa 8:00 mchana, Mwenyekiti wa ACT
Wazalendo, Anna Mghwira akiwa na viongozi wenzake, isipokuwa Kiongozi wa
Chama, Zitto Kabwe alikuwa mbele ya kamera za wanahabari akifafanua
kilichotokea kwa wanachama, wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa
ujumla.
Alisema ilipotimu saa 4:00 asubuhi
walipewa taarifa na mwenye ukumbi kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni
limemjulisha kuwa chama hicho hakina kibali cha kuendesha kongamano
hilo na kwamba kisiruhusiwe kufanya hivyo.
“Huku ni kufifisha demokrasia. Wapigania haki za kiraia wasimame imara na vyama vya upinzani katika kuilinda,” alisema Mghwira.
Wakati kongamano hilo likizuiwa, kuna
taarifa za kukanganya juu ya alipo Zitto baada ya kudaiwa alikuwa
anasakwa na polisi tangu juzi.
Taarifa hizo zinakuja siku chache
baada ya kiongozi huyo kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es
Salaam na kuhojiwa juu ya kauli alizozitoa kwenye mkutano wa hadhara
zinazokosoa utendaji wa Serikali na kupinga matokeo ya uchaguzi wa
Zanzibar.
Baadaye jioni, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa alitoa taarifa kuwa Zitto ametoweka na hajulikani alipo. Hiyo ilikuwa ni baada ya askari kanzu kumtafuta kwa muda kwa saa kadhaa.
“Zitto amekuwa akitafutwa kwa muda
mrefu. Askari wanalinda nyumbani kwake tangu jana (juzi) usiku. Hivi
sasa ametoweka, hatujui alipo. Lolote litakalompata, Jeshi la Polisi
litajibu,” alisema Mtemelwa.
Awali, Mghwira alipoulizwa imekuwaje kuhusu Zitto alijibu kuwa mkutano ulikuwa wa dharura ndiyo maana viongozi wote hawakuwapo