NI miaka mingi sasa tangu
utaratibu wa mabasi ya abiria kusafiri usiku ulipositishwa miaka ile ya
mwanzoni mwa tisini. Sababu kubwa iliyotolewa wakati huo ni kudhibiti
ajali, kwani madereva walionekana kuzidiwa na usingizi.
Kuanzia wakati huo, iliamriwa mabasi
yasafiri mchana na ikifika saa nne usiku, popote yalipo, yasimame ili
kusubiri kukuche tayari kuendelea na safari zake. Imekuwa hivyo tangu
hapo na inaendelea, hakuna dalili kama kuna mabadiliko yatatokea.
Udhibiti wa ajali hata hivyo, ambayo
ndiyo ilikuwa sababu kubwa, haikuonekana kupatiwa dawa, kwani
ziliendelea kutokea hata mchana na kuleta madhara makubwa kwa watu na
mali zao, kiasi kwamba wakati fulani, ikatolewa amri nyingine ya mabasi
yote kufungwa kitu kilichoitwa Speed Governor, ili kudhibiti mwendokasi
wa mabasi hayo, jambo ambalo nalo lilifeli.
Katika hali halisi ya mazingira ya
Tanzania kwa sasa ni vigumu kutoa sababu moja pekee, kwamba ndiyo
inayosababisha ajali za magari, achilia mbali mabasi. Lakini pia, ni
vizuri kutazama uwiano wa faida na hasara za kufutwa kwa safari hizi za
mabasi nyakati za usiku.
Wakati katazo hili linatolewa,
miundombinu ya barabara nyingi ilikuwa mibovu, tofauti kabisa na sasa
ambapo karibu miji mikubwa yote imeunganishwa kwa lami. Wakati ule wa
zamani, hakukuwa na check points za usalama barabarani, tofauti na sasa
ambapo zipo za kutosha kila baada ya umbali kadhaa.
Katika nchi ambayo kasi ya utendaji kazi
wa serikali imeongezeka, ikiwa ni pamoja na kuhimiza ulipaji wa kodi,
wafanyabiashara wadogo na wa kati, wanaotumia usafiri wa barabara
kufanikisha biashara zao ni wadau muhimu wanaopaswa kuangaliwa na
utaratibu huu wa kupiga marufuku mabasi kusafiri usiku.
Na siyo wafanyabiashara tu, lakini hata
raia wa kawaida, kwa nini wasisafiri usiku ili asubuhi waamke waendelee
na kazi? Usafiri wa miji kama Arusha, Moshi, Dodoma, Singida, Iringa,
Mbeya, Ruvuma, Lindi, Mtwara kwenda Dar es Salaam na kinyume chake ni
ndani ya saa 12 tu. Kwa nini sheria zisiboreshwe ili mabasi yasafiri
usiku?
Kwa mfano, mabasi yawe na madereva
wawili kwa ajili ya kupokezana kwa uchovu na usingizi, lakini pia
wapimwe kabla ya kuanza safari kama wametumia kilevi na zile check
points ziwe imara kukagua mwendokasi.
Tunapotaka Tanzania ya viwanda na kuipa
nguvu kauli mbiu ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu, ni lazima pia
tufanye kazi kwa saa 24 kwa kadiri inavyowezekana. Dunia yote ndivyo
inavyokwenda, mtu asafiri wakati wowote kwa kutumia mabasi.
Kufanya mwisho wa mabasi kusafiri ni saa
nne usiku, ni kurudi nyuma wakati tunataka kusonga mbele, kitu cha
msingi mamlaka zinazohusika zifanye kazi zao kwa weledi na uaminifu,
mchana tufanye kazi Dodoma, usiku tusafiri, asubuhi tuibukie kazini Dar
es Salaam!
Nachochea tu!