Frank Mvungi-Maelezo.
Serikali
imeanza kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ( TEHAMA) katika
kutangaza nafasi za kazi,kupokea maombi,kuwaita waombaji kazi kwenye
usaili na kuwawezesha kutumia teknolojia hiyo kupata ajira.
Kauli
hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini toka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira Bi
Riziki Abraham wakati wa mkutano na Vyombo vya Habari uliolenga kueleza
mikakati ya Serikali kuboresha mfumo wa kupokea maombi ya ajira na
kuyashughulikia.
“Sekretarieti
ya Ajira inatoa rai kwa waombaji fursa za Ajira kujisajili katika mfumo
wa Ajira unaopatikana kupitia anuani ya tovuti ya www.ajira.go.tz na
mfumo wa” job alert system” au kupitia simu za kiganjani kwa kupiga
*152*00# ili kuomba fursa za ajira zinazopatikana” Alisisitiza Riziki.
Akifafanua
kuhusu faida za kutumia TEHAMA kuendesha mchakato wa ajira, Riziki
amesema kuwa mfumo huo unasaidia kupunguza idadi ya siku za kuendesha
mchakato wa ajira kutoka siku 90 hadi 52 kwa sasa.Aliongeza faida
nyingine kuwa ni Serikali inapanua wigo wa utoaji taarifa za uwepo wa
fursa za Ajira hasa kwa waombaji wa ajira waishio vijijini.
Alisema
mfumo huu unalenga kupunguza changamoto kadhaa zikiwemo malalamiko ya
baadhi ya waombaji fursa za ajira kuhusu upotevu wa maombi yao ya
kazi.Hadi kufikia Mei, 2016 jumla ya waombaji wa fursa za Ajira
waliokuwa wamejiandikisha kwenye mfumo wa utumaji maombi ya kazi
walikuwa (97,765).
Aidha
jumla ya waombaji wa fursa za Ajira 89,484 wamejiunga kwenye mfumo wa
kupata taarifa za uwepo wa fursa za Ajira kupitia simu za kiganjani.