
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati),
akiongea jambo na Balozi wa Jamhuri
ya Watu wa China, Dkt. Lu Youqing (wa pili kushoto) wakati alipomtembelea ofisini kwake jijini
Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Afisa
Ubalozi wa China.

Balozi wa wa Jamhuri ya
Watu wa China, Dkt. Lu Youqing (katikati) akimweleza jambo Afisa Ubalozi wa
China nchini, wakati wa kikao chake na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (kulia).

Afisa Ubalozi wa China nchini (wa kwanza kushoto) akimweleza jambo
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo wakati wa kikao chake na
Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dkt. Lu Youqing (katikati).

Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dkt. Lu Youqing (wa tatu
kushoto), akimweleza jambo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Utumishi Wizara ya
Nishati na Madini, Lusias Mwenda. Wengine ni ujumbe ulioambatana na Balozi wa
China.
Na Asteria Muhozya, Dar
es Salaam.
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa
China imeitaja nchi ya Tanzania kuwa na nafasi kubwa ya kunufaika na fedha
kiasi cha Dola Bilioni 60 kupitia uwekezaji sekta ya nishati, fedha zilizoahidiwa
kutolewa na nchi hiyo wakati wa Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano baina
ya China na Afrika, uliofanyika nchini Afrika Kusini mwezi Desemba,2015.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar
es Salaam na Balozi wa China nchini, Dkt. Lu Youqing na ujumbe wake alipokutana
na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake jijini
Dar es Salaam na kuongeza kuwa, China ina imani kubwa na Rais wa Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna anavyosimamia masuala mbalimbali
nchini, pia Profesa Sospeter Muhongo kutokana na namna anavyoisimamia sekta ya Nishati na Madini.Miongoni mwa Sekta zinazopewa
kipaumbele katika fedha hizo ni pamoja na pamoja na miundombinu, afya, biashara, uwekezaji na
kupunguza umaskini, barani Afrika.
Kutokana na mahusiano mazuri
ambayo yamekuwepo kwa miongo kadhaa baina ya nchi hizo mbili, Balozi Youqing amemwakikishia
Waziri Muhongo kuwa, China itaendeleza ushirikiano huo kwa kuhakikisha inazishawishi
kampuni kubwa na zilizobobea kitaalamu na kiteknolojia za China, ili ziweze kushirikiana
na Tanzania katika sekta ya nishati, na zaidi katika uzalishaji umeme kwa
kutumia Makaa ya Mawe kutokana na namna ambavyo Wizara inavyokipa kipaumbele chanzo
hicho kuzalisha umeme nchini.
Wakati huo huo, China imesema
itaendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi Watanzania kusoma masuala ya
mafuta na gesi katika vyuo mbalimbali nchini humo kutokana na umuhimu wa sekta
hiyo na kwamba, China inapenda Tanzania ifanikiwe katika kuzalisha wataalam wa
kutosha katika fani hizo na kuongeza kuwa, anatambua juhudi zinazofanywa na
Waziri Muhongo kuhakikisha wanafunzi wengi wa kitanzania wanapata fursa ya
kusoma masuala ya mafuta na gesi maeneo mbalimbali Duniani, ikiwemo China.
Aidha, leo tarehe 26 Februari,
2016, Wizara ya Nishati imetangaza nafasi za Masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania
kuomba kusoma katika Vyuo vya China katika fani za Mafuta na Kazi katika ngazi za
Shahada ya Uzamili (Masters) na Uzamivu (Phd). Maelezo zaidi ya kuomba nafasi
hizo yanapatikana kupitia tovuti ya wizara www.mem.go.tz