
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa taarifa ya siku 100 za kwanza za Serikali ya awamu ya tano.
TAARIFA YA SIKU 100 ZA KWANZA ZA SERIKALI YA
AWAMU YA TANO ILIYOTOLEWA NA
BALOZI OMBENI Y. SEFUE, KATIBU MKUU KIONGOZI,
IKULU, TAREHE 12 FEBRUARI, 2016
__________________________
Utangulizi
Serikali
ya awamu ya Tano imetimiza siku 100 tangu iingie madarakani tarehe 5 Novemba,
2015. Japo siku 100 ni chache sana kufanya tathmini ya kina, zinatosha kuonesha
muelekeo wa serikali na kupata kionjo cha uthabiti wa dhamira yake ya
kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.
Kumekuwa na shauku kubwa ya wananchi
kujua kilichofanywa na Serikali hii katika siku zake 100 za mwanzo. Ni shauku
ya haki ambayo sisi katika Serikali hii lazima tujaribu tuwezavyo kuikidhi.
Ndio maana kuanzia juzi Mawaziri mbalimbali wanazungumzia mafanikio katika hizo
siku 100, kila mmoja akienda kwa undani kwenye sekta yake. Nawaomba wananchi
wafuatilie kwa karibu yale ambayo Mawaziri hawa wanayatolea taarifa kwenu ikiwa
ni sehemu ya uwajibikaji wao kwa wananchi.
Mimi pia, kwa nafasi yangu ya Katibu
Mkuu Kiongozi, ambaye ni Katibu wa Baraza la Mawaziri na Mkuu wa Utumishi wa
Umma, nimepokea maswali mengi ya waandishi wa habari na wananchi wengine kuhusu
siku 100 za kwanza za uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Maeneo yanayohusu sekta mbalimbali yatazungumzwa na Mawaziri wanaohusika.
Lakini nimeona baadhi ya maswali yanaweza kujibiwa tu na ofisi hii, yaani
Ikulu.