MGOMBEA
urais wa CCM, Dk John Magufuli amewataka wananchi kumchagua ili awe
rais wa tano ajaye wa Tanzania huku akiahidi kushughulikia masuala
mbalimbali ya wananchi na hivyo kuliletea Taifa maendeleo kwa muda wote
atakaokuwepo madarakani.
Akizungumza
na wananchi wa mkoani Lindi katika muendelezo wa kampeni zake, Dk
Magufuli alisema akichaguliwa kushika nafasi hiyo, pamoja na mambo
mengine atakayoyafanya atatumia utajiri wa gesi uliopo katika mikoa ya
Kusini, kutoa ruzuku kwa vifaa vya ujenzi ili kushusha bei na
kuwawezesha wananchi kujenga nyumba bora.
Amesema
pia atatumia nafasi hiyo kutafuta namna bora ya kuwainua wakulima wa
korosho, tofauti na utaratibu wa sasa wa stakabadhi ghalani, alisema
umekuwa ukiwasababishia umasikini mkubwa wakulima wa zao hilo.
Akiwa
Nachingwea, Ruangwa, Mtama na Lindi Mjini, Dk. Magufuli alisema tofauti
na wapinzani wanaoahidi kuondoa nyumba za nyasi na tembe nchi nzima kwa
siku 100 watakazokaa Ikulu, jambo alilosema ni ndoto, Serikali yake
itakachofanya ni kushusha bei ya mabati, saruji, nondo, misumali na
vifaa vingine vya ujenzi ili wananchi wajenge nyumba bora.