Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Mjumbe wa Kamati ya Kampeni, January Makamba.
CCM itafunga kampeni zake kwa utaratibu mpya na
kwa kishindo. Kampeni za CCM zitafungwa kitaifa kwa mikutano mikubwa ya
kampeni katika mikoa mitano. Mikutano hiyo itaongozwa na viongozi wa CCM
kitaifa waliopo madarakani na wastaafu. Mikoa hiyo na viongozi
wakaoongoza mikutano hiyo ni kama ifuatavyo:
1. Mwanza – Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa CCM, Dkt.
John Pombe Magufuli, Mgombea Urais, na Ndugu Samia Hassan Suluhu,
Mgombea Makamu wa Rais
2. Tanga – Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM
3. Mbeya – Ndugu Benjamin William Mkapa, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
4. Mtwara – Ndugu Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
5. Kigoma – Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
6. Kilimanjaro – Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu
7. Mara – Ndugu Joseph Warioba, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu
Kati ya leo na kesho, maeneo mengine yanaweza kuongezeka. Mikutano
hii itaanza saa sita mchana na itarushwa, yote kwa pamoja, kwa matangazo
ya moja kwa moja ya vituo vya televisheni vitano na vituoa vya redio
67. Vilevile, watakaohudhuria katika mikutano hii wataunganishwa moja
kwa moja na mkutano wa Mwanza, alipo Mwenyekiti, Mgombea na Mgombea
Mwenza, na wataweza kusikiliza hotuba ya Dkt. Magufuli moja kwa moja
kupitia screens zitakazokuwa katika viwanjani vyote hivi saba.
Namna hii ya ufungaji wa kampeni itakuwa ni ya kihistoria, na
inadhihirisha nguvu ya CCM inayoiwezesha kufanya mikutano mikubwa ya
kampeni kwa siku moja katika maeneo mbalimbali nchini. Lakini pia
tutafanya historia katika tasnia ya utangazaji wa televisheni hapa
nchini kwa kutangaza na kuunganisha kwa pamoja matukio saba kwa wakati
mmoja.
Kwa upande wa Dar es Salaam, tutafanya mkutano mkubwa wa ufungaji
wa kampeni za Mkoa wa Dar es Salaam, katika Uwanja wa Jangwani, kesho,
Ijumaa, tarehe 23 Oktoba 2015. Siku ya Jumamosi, tarehe 24 Oktoba 2015,
Wagombea Ubunge katika majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam watafunga
kampeni katika maeneo ya majimbo yao kwa namna mahsusi.
Tathmini ya Kampeni Kama Chama, tumeridhika na ubora na ukubwa wa
kampeni tulizofanya licha ya changamoto za hapa na pale. Dkt. Magufuli
na Ndugu Suluhu wamefanya kazi kubwa, na kwa bidii kubwa, na maarifa
makubwa. Wamekuwa barabarani kwa siku 57 wakifanya mikutano kati ya 8
hadi 12 kwa siku. Imani yetu ya ushindi inatokana na kazi kubwa
waliyofanya. Pia, CCM inawashukuru viongozi, wapenzi wa washabiki wake –
wa makundi mbalimbali ya kijamii - kote nchini kwa kazi kwa kazi kubwa
ya kampeni waliyoifanya.
Kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanyika, na kutokana na
mwenendo wa tafiti huru na tafiti zetu za ndani, CCM inategemea ushindi
wa asilimia zisizopungua 69.
Uchaguzi wa Amani
CCM haitachoka kuendelea kusisitiza uchaguzi wa amani na utulivu.
Sisi kama chama kikubwa cha siasa nchini, chenye wafuasi wengi zaidi, na
chenye dhamana ya uongozi wa dola, tutatimiza wajibu wetu wa kuhimiza
utulivu kwa wapenzi, washabiki na wanachama wetu. Tunawataka na wenzetu
wafanye hivyo.
Kauli za wenzetu kwamba kura zitaibiwa ni kauli za kutojiamini na
kujiandaa kufanya vurugu. Kauli za kwamba washabiki wa UKAWA wakishapiga
kura wabaki vituoni kulinda kura si kauli za wanaotaka uchaguzi wa
amani.
Kwa utaratibu wetu wa uchaguzi, utaratibu wa pekee kwa Chama
kulinda kura zake ni kwa kupitia wakala wa vyama waliopo kwenye kila
kituo cha kupiga kura na wenye nguvu na mamlaka ya kisheria ya
kushuhudia zoezi zima, kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura hadi kutangaza
matokeo. Kura zinapigwa na kuhesabiwa vituoni mbele ya wasimamizi wa
uchaguzi, mawakala wa vyama na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya
nchi.
Mawakala wa vyama na wasimamizi wa uchaguzi wanaweka sahihi kwenye
fomu za matokeo, na matokeo hayo yanatangazwa na kubandikwa kwenye
kituo. Kwenye kituo kikuu cha Tume cha kujumlisha matokeo, mawakala wa
vyama pia huwepo na Tume hujumlisha matokeo kutoka kwenye fomu za
matokeo za vituo vya nchi nzima zilizosainiwa na mawakala wa vyama
kwenye kila kituo. Kwa viongozi wa UKAWA kuwaambia watu waingie
barabarani au kuvizunguka vituo vya kupigia kura eti ili kulinda kura
hakuna maana yoyote zaidi ya kutafuta namna ya kuhalalisha vujo, vurugu
na uporaji na kuwazuia watu wengine, hasa wanawake, kupiga kura.
Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama vizuie hili jambo kwasababu
halina nia njema.
Mkakati wa UKAWA ni kufanya vurugu baada ya kushindwa na
kutengeneza mazingira ya mgogoro wa kisiasa ili Jumuiya ya Kimataifa
iingilie kati na kupendekeza kugawana madaraka. Mkakati huo
hautafanikiwa. Tunaviomba vyombo ya ulinzi na usalama vihakikishe ulinzi
na usalama wa watu wote na mali zao siku ya uchaguzi na baada ya
uchaguzi.
CCM haitakubali hata kidogo ushindi wake kuhojiwa au kutiliwa shaka kwasababu tu ya vurugu zilizoanzishwa na watu wengine.
Siku ya Jumamosi, CCM itatangaza namba maalum za simu kwa
Watanzania wote ili siku kabla ya uchaguzi, siku ya uchaguzi na mara
baada ya uchaguzi, waweze kupiga simu au kutuma ujumbe pale watakapokuwa
wanabaini au kushuhudia vitendo vya kuvuruga amani na kuvuruga
utaratibu mzima wa uchaguzi.
Kupokea Matokeo
CCM imeweka utaratibu wa kupokea matokeo kwa kutumia mawakala wake
moja kwa moja vituoni na kupitia mtandao wa Chama. CCM inategemea kuwa
na matokeo ya uchaguzi nchi nzima ifikapo saa nne usiku, siku ya
uchaguzi, tarehe 25 Oktoba 2015.
Imetolewa na:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
22 Oktoba 2015
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
22 Oktoba 2015