
Ndugu zangu,
Nionavyo, Nchi yetu iko katika hali ya kama mgonjwa anayetafuta mawili makubwa; nafuu na uimara wa afya yake.
Kama
upepo kinzani hautalizuia taifa letu katika kusonga mbele, basi, miaka
ijayo itakuwa ni miaka ya ' Nchi kuanza kuwa na kukua zaidi' kutoka hali
ya sasa. Nchi itarajie mabadiliko makubwa hata kwenye mitazamo yetu
kuhusu kazi na nidhamu ya kazi hususan kwa watendaji.
Hata
hivyo, kwenye hali ya mgonjwa kuelekea kuitafuta nafuu na uimara wa
afya, uwezo , njia na mbinu za waganga zaweza kutofautiana. Uchaguzi ina
maana pia ya kumtafuta yule mganga mwenye kuonyesha kuwa na uwezo, njia
na mbinu za kuipata nafuu na uimara wa afya ya mgonjwa.
Hivyo,
tukiwa sasa, kama taifa zima, na tunapoelekea kwenda kulijenga daraja
kati ya jana na kesho, ni muhimu tukaitazama Tanzania kwanza na kuwa na
mioyo ya kuvumiliana na kuheshimiana. Umuhimu wa kuilinda amani yetu.
Ndugu zangu,
Katika
kuishi kwangu nina bahati ya kuwa na uzoefu wa miaka mingi wa
kufuatilia siasa za kitaifa, bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Katika
kuishi kwangu pia, sijawa na wala sifikirii kuja kuwa mwanachama wa
chama cha siasa. Kwangu Watanzania wa vyama vyote, na wasio na vyama ni
ndugu zangu. Na kwa kusema hivyo haina maana sina itikadi ya kisiasa
inayoniongoza. Mimi naamini katika Ujamaa na Kujitegemea. Ndio, I am a
Social Democrat.
Nilichokiweka
mezani jana ni mtazamo wangu. Sijarudi nyuma hata robo hatua.
Nimesimama pale pale, kwamba ninachokiona ni kuwa Serikali inayokuja ya
Awamu ya Tano itaundwa na John Pombe Magufuli.
La
Magufuli kuunda Serikali ishara zake niliziona muda mrefu na nikaweka
bayana hilo mwezi uliopita. Na leo zikiwa zimebaki siku tatu kabla
kufanyika Uchaguzi Mkuu, hakika sizioni ishara mpya.
Kwanini John Magufuli atashinda?
Kuna
sababu moja kubwa. Kwamba wakati mgombea wa Ukawa- Chadema anabebwa na
umaarufu aliokuwa nao akiwa CCM, umaarufu huo wa mtu mmoja umekuwa wa
gharama kwa Chadema kama chama.
Ni
kwa vile, ilitarajiwa, na haikutokea, kuwa mgombea urais wa Ukawa-
Chadema angetoka CCM na kundi kubwa la wafuasi kutoka CCM. Kwa sasa
wachache waliohama CCM na Edward Lowassa wako katika kundi la '
Political spent forces'. Ni waliokwishatumika kisiasa kwa sifa ya mazuri
na mabaya.
Kabla
ya kuhama kwao hawakuwa kwenye nafasi za juu kwenye chama na Serikali,
na kuhama kwao kunaweza pia kutafsiriwa kuwa ' Wamechoshwa na masengenyo
ya ndani ya chama'.
Kwamba
chama chao kilishindwa kuwaonyesha umuhimu wao. Ndio, kumekuwa na kundi
la ' Wanasiasa wanung'unikaji' ambao wangetimiziwa haja zao za kisiasa
wangebaki huko huko CCM na wangesimama majukwaani kuimba ubora wa CCM !
Ni
kweli kuwa, kwenye siasa umaarufu wa mgombea ni jambo muhimu, lakini,
sadaka za kisiasa huambatana na umaarufu wa chama na kukubalika kwake
kwa wananchi.
Kwa
ajenda ya kupambana na ufisadi ambayo Ukawa- Chadema walikuwa nayo
mpaka miezi kadhaa iliyopita, kimsingi iliwajengea umaarufu na
kukubalika kama chama. Ni jambo la ajabu sana kuwa upinzani ukiongozwa
na Chadema umeitupilia mbali ajenda hiyo.
Ziada
ya matatizo ya upinzani kwa sasa ni hali ya kutoelewana kwa viongozi
wakuu ndani ya upinzani. Hali ya hata kugombania majimbo na kata. Na
kujiweka pembeni kwa Dr Slaa na Profesa Lipumba ni pigo kubwa.
Ina
tafsiri ya upinzani kupoteza sehemu kubwa ya mtaji wa imani kutoka kwa
wapiga kura. Upinzani umeshindwa kuonyesha mshikamano wa kiuongozi-
Cohesive leadership.
Wapiga
kura wanaelewa kuwa uongozi wa juu wa nchi ni jambo muhimu na nyeti.
Linahusu mustakabali wa nchi na maisha yao. Kwa viongozi wa upinzani
kushindwa kuonyesha cohesive leadership hakuwapi imani wapiga kura walio
wengi kuwa mambo yatakuwa shwari watu hao hao wakipewa nafasi ya
kuongoza nchi.
Na
ujio wa Edward Lowassa Ukawa- Chadema umeliibua kundi lingine la '
Wanung'unikaji' ndani ya UKAWA. Hawa wanahoji taratibu za Lowassa
kuingizwa Ukawa na kupewa nafasi ya juu ya kugombea urais. Ikumbukwe, Dr
Slaa na Profesa Lipumba wamejiengua, nao wana wafuasi wao.
Watanzania huchagua zimwi..
Chama
cha Mapinduzi katika Tanzania ni zaidi ya Chama cha siasa. Ni taasisi
kubwa na karibu kila Mtanzania ana nasaba na CCM. Ni moja ya vyama
vikongwe Afrika vyenye sifa kubwa ya kuwa na mizizi katika kila eneo la
ardhi ya nchi wanakoishi watu. CCM ni sehemu ya maisha ya Watanzania.
Ni katika uhalisia huo, kuna wanaokipenda chama hicho na kuna wanaokichukia pia, kwa wenye kukichukia kwao ni zaidi ya zimwi, ni kama shetani anayewawekea giza kwenye maisha yao. Watu hawa hulilia mabadiliko, na kwao tafsiri ya mabadiliko ni kuiondoa CCM tu, basi. Hawa si wengi sana kama inavyodhaniwa, lakini, wana uwezo mkubwa wa kupiga kelele ambazo CCM hawapaswi kuzipuuzia.
Ni katika uhalisia huo, kuna wanaokipenda chama hicho na kuna wanaokichukia pia, kwa wenye kukichukia kwao ni zaidi ya zimwi, ni kama shetani anayewawekea giza kwenye maisha yao. Watu hawa hulilia mabadiliko, na kwao tafsiri ya mabadiliko ni kuiondoa CCM tu, basi. Hawa si wengi sana kama inavyodhaniwa, lakini, wana uwezo mkubwa wa kupiga kelele ambazo CCM hawapaswi kuzipuuzia.
Na
hakika, katika kero na matatizo mengi wanayoyapata Watanzania, hufika
mahali wapiga kura wengi wanajua kuwa wanakwenda kuchagua zimwi.
Kwa
tabia, wapiga kura huwa ni waoga sana kuchagua wasichokijua. Na wanajua
pia, kuwa Rais wa nchi ni nafasi nyeti. Kama hawawajui watakaomzunguka
Rais, basi, huingiwa na mashaka.
Wahenga
walisema; " Zimwi likujualo halikuli likakwisha". Hivyo, Wapiga kura
wengi kwa tabia huenda kuchagua zimwi wanalolijua, na hapa ni CCM.
Edward Lowassa angehama na ' Mazimwi' mengi kutoka CCM, tena yale ambayo wapiga kura wanayajua, basi, nafasi ya Edward Lowasa kushinda urais ingekuwa kubwa.
Edward Lowassa angehama na ' Mazimwi' mengi kutoka CCM, tena yale ambayo wapiga kura wanayajua, basi, nafasi ya Edward Lowasa kushinda urais ingekuwa kubwa.
Mimi
naamini, Lowassa angebaki kuwa mgombea ndani ya CCM, bado Lowassa na
CCM wangeshinda , lakini kwa tabu sana kwa mantiki ile ile ya mgombea
kuzungukwa na mazimwi mengi ambayo wapiga kura wanayajua. Lakini,
upinzani ungepata viti vingi zaidi kuliko ambavyo itapata kwenye
uchaguzi ujao, ni kwa vile, upinzani ungebeba ajenda ya kupambana na
ufisadi ambayo ni kero kubwa kwa Watanzania wengi. Na nchi yetu
inahitaji siasa za upinzani kuanzia kwenye udiwani hadi ubunge.
Vinginevyo, kwa hali ninavyoiona sasa, Watanzania tutarajie ujio wa Serikali ya John Pombe Magufuli kama Rais wa Awamu ya Tano.
Ni mtazamo wangu.
Maggid,
Iringa.
Iringa.