Waziri wa Chakula na Kilimo Stephen Wasira na Ester Bulaya.
Akizungumza na
Mwananchi kwa simu jana, Wasira alisema hakuwahi kuvutana na Bulaya na
kwamba, kitendo chake cha kuhamia Chadema, kimempotezea mashabiki wengi
hususan vijana wa Jimbo la Bunda mkoani Mara.
Hata
hivyo, Bulaya alipoulizwa kuhusu hilo alisema kuhama kwake CCM
kumemrahisishia kupata wafuasi wengi wakiwamo vijana na wazee huku,
akidai kupigiwa simu mara kwa mara za kupongezwa kwa uamuzi wake wa
kujiunga Chadema.
“Tangu nilipokuwa CCM, nilikuwa
mwakilishi wa vijana na huku Chadema ndiyo kwenyewe, nimeendelea kuiteka
Bunda tofauti na awali,” alisema Bulaya.
Alisema
hakuwahi kufikiria uamuzi wa kukodi wananchi ili wahudhurie kwenye
mikutano yake, bali uhusiano bora kati yake na wakazi wa Bunda ndio
uliosababisha umati wa watu kufurika katika mkutano uliofanyika juzi.
Wasira: Bulaya si saizi yangu
Wasira
ambaye pia ni Mbunge wa Bunda (CCM), alisema vijana wengi wa jimbo hilo
walikuwa wanampenda Bulaya kwa sababu alikuwa CCM ambayo ndiyo chama
kilichomlea kisiasa hadi hapo alipofikia hivi sasa.
“Mfano
mzuri ni juzi katika mkutano wake uliovunja rekodi ya kuhudhuriwa na
watu wengi, wananchi waliletwa kwa malori kutoka sehemu mbalimbali
zikiwamo Mwanza na Serengeti,” alisema Wasira ambaye ameomba kuteuliwa
kugombea jimbo hilo kwa mara nyingine.
Alidai kuwa
Chadema imekuwa ikijinasibu kuwa haiwezi kukodisha wananchi kuhudhuria
katika mikutano yao, lakini juzi ilikuwa hivyo.
Akizungumzia
hali ya ushindani iliopo kwa wagombea waliojitokeza na kuchukua fomu ya
kugombea jimbo la Bunda, Wasira alisema upo kiasi na endapo CCM
itampitisha tena, yupo tayari kupambana na yeyote kutoka upinzani hata
Bulaya ambaye si saizi yake.
Bulaya: Wasira si saizi yangu
“Kizuri
kinajiuza bwana, sikuwa na sababu ya kukodi watu waje kushiriki kwenye
mkutano wangu, yeye na chama chake ndio wenye tabia hiyo. Hata hivyo,
wataambulia patupu safari hii,” alisema Bulaya.
Bulaya
alipouulizwa endapo Chadema ikimpitisha kuwania Bunda ataweza kupambana
na mgombea kutoka chama chake za zamani akiwamo Wasira, alijibu:
“Sioni
‘saizi’ yangu kati ya wote waliojitokeza kuchukua fomu ya Bunda, ni
bora Wasira akapumzika kwani kizazi chake kwa sasa hakipo.”
Katika hatua nyingine; Wasira amekanusha taarifa kuwa amempiga Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mara, Chistopher Sanya.
Wasira
alikiri kutokea kwa ubishi wa kawaida kati yake na Sanya, lakini siyo
wa kufikia hatua ya kupigana na kwamba, wanaosambaza taarifa hizo wana
lengo la kumchafua kisiasa.
chanzo: MWANANCHI
