WAKATI Tanzania ikiwa katika vuguvugu la kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25, 2015, kuliibuka mambo mengi ya kushangaza yaliyoongeza msisimko kwenye mbio za uchaguzi huo na kuonekana kuwa za kipekee zaidi kiasi cha kufuatiliwa kwa ukaribu na watu wengi kuliko chaguzi zilizopita.
LOWASSA ALITAJWA MARA NYINGI
Taasisi mbalimbali zilifanya utafiti na
kuibuka na wagombea wao, lakini jina la waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa lilitajwa mara nyingi na maeneo mengi, zikiwemo taasisi na
mitazamo ya watu mitaani.
MAKUNDI YA DINI YALIZIDISHA MATUMAINI
Moja kati ya mambo ya kusisimua ni lile
la kuibuka kwa baadhi ya manabii au viongozi wa makanisa nchini, wakidai
wameoneshwa na Mungu kuwa baadhi ya viongozi waliotangaza nia watakuwa
marais kutokana na maono yao.
Manabii hao waliibuka huku kila mmoja
akiwatangazia waumini wake kwamba, mgombea fulani ndiye atakuwa rais
2015, hali iliyowafanya wenye akili wachache wawapuuze baada ya
kujiuliza kwamba inawezekanaje Mungu akawatabiria watu tofauti kwa cheo
kimoja cha urais?
Wafuatao ni baadhi ya manabii waliowahi kuweka wazi wagombea wao kwa nyakati tofauti kwa maneno ya kuoneshwa kimaono:
Basileus Ezekiel Mabumba
Ni Mchungaji wa Kanisa la Last Glory.
Huyu aliwashangaza watu baada ya kuwa kiongozi wa kwanza wa dini
kufunguka kuwa, ameoneshwa na Mungu kwamba Edward Lowassa atakuwa rais
na kuweka msisitizo kwa kiapo kizito kuwa auawe kama hayo hayatatimia.
Askofu John Komanya
Kwa sasa ni marehemu, apumzike kwa
amani. Yeye alikuwa Askofu wa Huduma ya Cathedral of Joy (CoJ) ya
Kiluvya jijini Dar. Enzi za uhai wake alisema ameoneshwa na Mungu kuwa,
Lowassa atakuwa rais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Nabii Josephat Mwingira
Yeye ni Nabii wa Huduma ya Efatha yenye
makao yake makuu, Mwenge, Dar. Aliwahi kusema amepokea maono kutoka kwa
Mungu kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu atashinda
kinyang’anyiro cha urais na kusisitiza kuwa, hakuna wa kumzuia kwa
sababu ukuu umeamriwa juu yake. Lakini Nyalandu naye kama Lowassa
alitolewa katika hatua za mwanzoni.
Nabii Yaspi Bendera
Huyu ni Nabii wa Huduma ya The
Revelation Church iliyopo Buza Kipera, Dar ambapo naye aliwahi kutabiri
kwamba, Lowassa atashinda kwa kutumia maono yake na utafiti wa Taasisi
ya Twaweza uliobainisha kuwa, Lowassa ameongoza ushindi akifuatiwa na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda huku Dk. Wilbroad Slaa akishika nafasi ya
mwisho. Utabiri huo umebuma.
Nabii David Mpanji
Huyu ni Nabii wa Huduma ya Maombezi ya
GMCL, Mbeya. Yeye alikuwa tofauti kabisa na wengine ambapo kwa upande
wake alimpaka mafuta Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba
kuwa atashinda na kuwa rais na kudai amemuona ana roho ya kuongoza.
Hivyo kwa mafuta aliyompaka lazima
atakuwa rais huku akimfananisha na Mfalme Daudi wa kwenye Biblia
alivyopakwa mafuta na Nabii Samuel na kuwa mfalme wa Israeli.
John Magufuli, kidedea
Pamoja na maono, utafiti na mitazamo,
hatimaye, Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli ameibuka kidedea kuwa
mgombea urais ndani ya chama chake cha CCM akiwaongoza wenzake 38
waliojitokeza kugombea nafasi hiyo.
Juzi, baadhi ya wasomaji wa gazeti hili
walizungumza na gazeti hili ambapo hoja yao kubwa ilikuwa ni swali la
manabii na wachungaji kutabiri mambo halafu yasitimie, wanakosea wapi?
GPL