Ili kupata mgombea mmoja CCM imekuwa
ikitumia vikao vyake vitatu, Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu (NEC) na
Mkutano Mkuu (GM) kumpata mwanachama mmoja wa kupeperusha bendera ya
chama hicho na ndiye atakayeshindana na wagombea wa kambi ya upinzani
ili kuingia ikulu.
Mfumo huo ambao umetumika kumpata
mgombea ndani ya chama katika uchaguzi wa mwaka 1995, 2000, 2005 na
2010, mwaka huu umebadilishwa kwani kulikuwa na kikao kingine cha Baraza
za Ushauri la chama hicho ambacho kilichuja utitiri wa wagombea na
kushauri kabla ya kufikisha kwenye vikao hivyo.
Uzoefu wa washauri hao katika madaraka,
hekima, busara na ukongwe katika duru za siasa umesaidia kuchambua
wagombea hao na kubakiza wachache wenye vigezo, taaluma na utendaji na
majina yao yakapelekwa Kamati Kuu na hatimaye Mkutano Mkuu wa CCM.
Baraza hilo linaloundwa na Mwenyekiti
wake, Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Katibu, Pius Msekwa
na wajumbe wake Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, marais
wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk. Salmin Amour pamoja na
Mzee John Malecela wamefanya kazi nzuri.
Baraza hilo lililoundwa kwa kanuni za
chama mwaka 2012, kwa kutumia uzoefu wa wanachama wake, kumbe huwa
linatumika kama chekecheke, dira, mwongozo na kioo cha kupata mgombea
safi na bora, tumeona Dodoma.
Wazee hao ambao wamebobea katika medani
za siasa walitakiwa kutoa mapendekezo juu ya ubora, uwezo, weledi wa
wagombea ndani ya chama ili kusaidia vikao vya chama, kwa kutumia hadidu
zao.
Washauri hao wa chama walitakiwa
kuwachambua na kuwajadili wagombea wote 38 waliojitokeza kuwania nafasi
ya urais kuanzia maisha yao katika jamii, chama na nchi kwa ujumla,
kabla majina yao na sifa zao pamoja na vigezo vya kuwapitisha kuyapeleka
majina yao mbele ya Kamati Kuu ya CCM.
Kwa wasiojua ni kwamba vikao vya chama
vilianza baada ya kupata hadidu za rejea kutoka Baraza la Ushauri la
chama, pamoja na nyaraka kutoka Kamati ya Usalama na Maadili na ndipo
Kamati Kuu ikafanya uamuzi wa kuteua watangaza nia watano, Januari
Makamba, Bernard Membe, Dk. John Magufuli, Amina Salum Ali na Dk.
Asha-Rose Migiro.
Kwa ujumla vikao vyote vya mchakato huo
havikuwa lelemama, kwanza kutokana na wingi wa wagombea waliojitokeza
kuwa na sifa, umahiri, ubora na uwajibikaji uliotukuka, ambapo ni kwa
mara ya kwanza wamejitokeza kwa wingi kutoka Bara na Visiwani.
Kazi ya kuchuja wagombea ilikuwa ngumu
lakini vikao vilifanya na kubakiza watatu wenye sifa stahiki ambao ni
Dk.John Magufuli, Dk. Asha-Rose Migiro na Amina Salum Ali.
Umakini wao katika kuteua wagombea bora
kutoka miongoni mwa idadi hiyo kubwa ya watangaza nia ambayo ni kubwa
mara mara nne ya wale 11 waliowania urais mwaka 2005, watakumbwa na
Watanzania kwa kitendo hicho cha ushujaa cha kukivusha chama salama.
Naamini baraza hilo la wazee lilikuwa
likimtegemea Mungu ili kuwasaidia kuangalia uwezo wa mgombea wa
kuongoza, taaluma yake ili kuwapa Watanzania rais bora wa awamu ya tano
atakayepokea mikoba ya Rais Jakaya Kikwete mara baada ya Uchaguzi Mkuu
utakapofanyika Oktoba 25, mwaka huu ambaye amejulikana kuwa ni Dk. John
Pombe Magufuli aliyepata kura 2104 sawa na asilimia 87.1.
Kilichobaki ni wana CCM wote kuungana na
kuondoa makundi ili ushindi upatikane na Dk. Magufuli awe rais,
anayeng’ang’ania makundi hatufai, atupishe.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
GPL