/caption]
KAMPUNI
ya Simu Tanzania (TTCL) leo imekabidhi mradi mkubwa wa Mkongo wa
Mawasiliano ambao umeyaunganisha matawi yote ya Bohari ya Dawa Nchini
(MSD) na Makao Makuu ili kufanya kazi zake kwa haraka na kwa ufanisi.
Hafla ya kukabidhi mradi huo imefanyika leo Makao Makuu ya Ofisi za MSD
zilizopo jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi mradi huo, kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk.
Kamugisha Kazaura, Ofisa Mkuu wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya Simu
Tanzania, Peter Ngota alisema kampuni hiyo inajisikia fahari kufanikiwa
kuunganisha ofisi zote za kanda za MSD na Makao makuu kupitia mkongo wa
mawasiliano ambao ni salama na wauhakika katika utendaji wa kazi.
Alisema MSD ni moja ya wateja wake wakubwa ambao wameunganishwa kihuduma
kupitia mkongo wa mawasiliano ambao ufanisi wake ni mkubwa na salama
kwa wateja tofauti na teknolojia nyingine za mawasiliano.
Alisema
huduma za mkongo wa mawasiliano zinazotolewa na TTCL kwa wateja wake ni
salama na zenye ubora katika ufanisi jambo ambalo limevuta idadi kubwa
ya wateja kuongezeka kila uchao.
Alisema kwa sasa TTCL inatoa huduma hizo kwa makampuni ya simu, taasisi
mbalimbali za umma na binafsi, mabenki, hospitali kadhaa, vyombo vya
habari, wateja binafsi pamoja na mataifa kama Rwanda, Burundi, Uganda,
Kenya, Zambia na nchi ya Malawi.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhiwa mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Cosmas
Mwaifwani alisema MSD ilianza kufungiwa mawasiliano ya mkongo Mwezi Mei,
2011 kwa kuunganisha ofisi za makao makuu na baadaye ofisi mpya za
mauzo zilizopo Muleba zilizounganishwa mwaka 2013.
Alisema MSD ilifanya uamuzi wa kuhamia kwenye teknolojia ya Mkongo baada
ya kuona uwepo wa matatizo makubwa yaliyokuwepo katika teknolojia ya
awali ambayo ni waya wa jadi yaani shaba ambayo pia ilitolewa na kampuni
ya TTCL.
"...Bohari
ya Dawa iliamua kuhamia katika teknolojia hii baada ya kufanya utafiti
wa kina na kuona faida ambazo zinaweza kupatikana kwa kutumia teknolojia
hii (mkongo) na hivyo kuachana na matatizo yanayosababishwa na
teknolojia ya shaba. Hii ina maana mkongo unaweza kubeba habari zaidi na
kwa ubora mkubwa kuliko waya wa shaba," alisema Mwaifwani.
Alisema
kwa sasa MSD imeanza kupata mafanikio makubwa baada ya kuanza kutumia
huduma za mkongo na tayari TTCL imeyaunganisha Ofisi 10 za MSD ambazo ni
Kanda nane (8) pamoja na vituo viwili vya mauzo; alizitaja Kanda
zilizounganishwa ni pamoja na Dar es Salaam, Moshi, Iringa, Mbeya,
Mwanza, Tabora, Dodoma, Mtwara, Muleba, Tanga, Makao Makuu ya Muda
Jamana na Ofisi za Keko Mwanga.
"...Tunasema
kwamba Bohari ya Dawa imedhamiria kuokoa maisha ya Watanzania kwa
kutumia teknolojia ya Mkongo yenye kasi zaidi, usalama, na gharama nafuu
zaidi katika kuhakikisha dawa zenye ubora zinamfikia kila Mtanzania kwa
wakati na kupunguza kero ya kusubiri huduma zetu kwa muda mrefu kwani
sasa huduma zinapatikana kwa wakati kwa kuwa teknolojia inayotumika ni
ya kisasa na yenye ubora wenye kukidhi viwango vinavyohitajika na bohari
ya dawa," alisema Mkurugenzi Mkuu, Mwaifwani.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
canzo JIACHIE