Dar/Dodoma. Ni wiki ngumu kwa Chama cha
Mapinduzi (CCM). Ndivyo unavyoweza kusema kwani chama hicho
kinachotawala kitafanya vikao vyake vya juu vitakavyohitimishwa kwa
kumpata mgombea wake wa urais.
Mchakamchaka utaanza na kikao cha Kamati ya
Maadili keshokutwa kukutana. Tayari CCM imetangaza kuwa itatumia vigezo
13 ilivyojiwekea kuwachambua wagombea 38 waliochukua na kurejesha fomu
ili kupata majina ya wachache watakaopigiwa kura na mkutano wake mkuu.
Awali, kulikuwa na watangazania 42 waliochukua
fomu za kuomba kuteuliwa na CCM, lakini wanne kati yao hawakurejesha
fomu. Kamati Kuu itakayokutana Alhamisi itakuwa na kazi ya kuwachuja
hadi kubakia wasiozidi matano yatakayopigiwa kura Ijumaa ijayo katika
Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kubaki matatu.
Katibu wa Baraza la Ushauri wa Wazee wa CCM, Pius
Msekwa juzi alilieleza gazeti hili kuwa mbali na sifa hizo, suala
jingine litakalotizamwa ni iwapo wagombea hao walikiuka kanuni na
taratibu za uchaguzi wakati wote wa mchakato.
Majina matatu yatakayopitishwa katika kikao cha
NEC ndiyo yatapigiwa kura na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM utakaokaa
Julai 11 na 12 na kupata mwakilishi mmoja wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba 25.
Uzoefu unaonyesha kuwa chama hicho huzingatia
mambo mengi katika kufanya uteuzi, ikiwa ni pamoja na kutafuta mtu
atakayeondoa makundi yaliyoundwa wakati wa uteuzi wa mgombea urais.
Baadhi ya mambo yanayotajwa kuwa yatakuwa karata
muhimu katika mchujo huo ni suala la Muungano, jinsia, eneo la
kijiografia, rekodi ya mtia nia na kukubalika kwa kada hasa katika
kipindi hiki ambacho upinzani umeimarika. Hofu inayoonekana kukikumba
chama hicho ni ya kumpata mgombea mwenye sifa na anayekubalika na
atakayeweza kukabiliana vyema na yule atakayesimamishwa na Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema,
CUF na NLD.
Kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho,
Rais Jakaya Kikwete kwamba hana mgombea anayemuunga mkono kinaonyesha
jinsi mchujo huo utakavyokuwa mgumu.
Kauli ya Takukuru
Kutokana na unyeti wa wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah
amesema vijana wake wako Dodoma na kuwatahadharisha wagombea wote
kuzingatia sheria.
“Nawashauri wagombea wote wazingatie Sheria ya
Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Kupambana na Rushwa, wafanye mambo
kistaarabu na ambaye atakwenda kinyume, sheria itachukua mkondo wake,”
alisema.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema jeshi hilo limejiandaa vizuri kwa ugeni huo mkubwa
“Natoa onyo kwa mtu yeyote mwenye nia ovu au kutaka kufanya
kitendo chochote cha kuhatarisha usalama, atashughulikiwa kwa nguvu zote
za kisheria,” alisema Misime.
Aliwataka wajumbe wa vikao hivyo, wageni na
wananchi kutambua kuwa usalama unaanza kwa kila mmoja wao, hivyo wakiona
jambo lolote linaloashiria uhalifu au si la kawaida, watoe taarifa kwa
vyombo vya ulinzi na usalama.
Wasiwasi wa kukosa vyumba
Huku zikiwapo taarifa za hoteli zote kujaa mapema, mmoja wa wagombea Boniface Ndengo, alisema,
“Mimi nataka niwepo huko (Dodoma) kuanzia Jumanne
jioni, nitajaribu kufanya mpango wa chumba lakini nimesikia vyumba
vimejaa, sijui kama nitapata nafasi,” alisema.
Alisema hataki kubeba watu wengi, bali ataongozana
na watu wasiozidi watatu na amepata habari kuwa wagombea wote
wataalikwa kwenye mkutano mkuu.
Taarifa zilisema kuwa CCM imechukua hoteli zaidi
ya 300 na hakuna wajumbe watakaochangia chumba kwa kulala wawili kama
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kauli ya wasomi
Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Idara ya
Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda
alisema katika uteuzi huo, ni vyema CCM ikamteua mwanachama
anayekubalika na ambaye atamudu hali ya upinzani iliyopo sasa.
“Upinzani wa sasa siyo sawa na wa miaka mitano
uliopita, wateue mtu atakayepata kura za pande zote kwa maana ya kura
ndani ya chama na nje ya chama,” alisema Mbunda.
Alitolea mfano wa kile kilichotokea nchini Kenya
wakati wa Kanu wakati chama hicho kiliposhinikiza mgombea fulani
apitishwe wakati hakuwa anakubalika.
“Wasishinikize mtu fulani apite. Lazima wazingatie
hayo ili kusije tokea mpasuko,” alisema na kuongeza kuwa binadamu
wapenda hisia zao zizingatiwe.
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly
Mbwete alisema CCM haikuwa na utaratibu mzuri tangu mchakato wa kuchukua
fomu za kuwania urais ulipoanza.
“CCM lazima iwe na utaratibu mzuri wa kumchagua
mtu au watu wachache watakaowania nafasi hiyo. Sasa tumeona kila mtu tu
anajitokeza kuchukua fomu ya kuwania urais. Huo siyo utaratibu mzuri,”
alisema Profesa Mbwete.
Alisema kutokana na hilo, inakuwa vigumu hata kutoa maoni juu mchakato wake wa kumteua mgombea urais.
Imeandikwa na Noor Shija na Sauwa (Dodoma), Fidelis Butahe na Suzan Mwillo (Dar).
