Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada ya kikao cha viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD, Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi kilichofanyika juzi, mambo kadhaa yameafikiwa na kama hakutokuwa na mabadiliko yoyote, mteule wa urais kupitia umoja huo atabainishwa.
Dar es Salaam. Baada ya vikao mfululizo wiki hii, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unatarajia kumtangaza mgombea urais wake kesho.
Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada
ya kikao cha viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD,
Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi kilichofanyika juzi, mambo kadhaa
yameafikiwa na kama hakutokuwa na mabadiliko yoyote, mteule wa urais
kupitia umoja huo atabainishwa.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi
alithibitisha kuwa tayari makubaliano ya kugawana kata na majimbo kwa
nafasi za udiwani na ubunge yamekamilika na kilichobaki ni utekelezaji.
“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata na
majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja na
hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” alisema Dk
Makaidi.
Siku chache baada ya baadhi ya wabunge kupewa
adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda, Jumanne ya
wiki hii Chadema ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo kadhaa ya
kitaifa.
Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi wa
waandamizi wa Ukawa walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja huo
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema
iliendelea na vikao vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao
cha Kamati Kuu ya Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha jina la
mgombea urais.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika
alithibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani vya chama hicho na kueleza
kuwa hawezi kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na
kwamba kesho taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.
“Kwa kifupi ni kwamba kikao bado kinaendelea.
Nimetoka mara moja tu kupokea simu yako. Mazungumzo yatakapokamilika
tutawajulisha (vyombo vya habari),” alisema Mnyika.
Mvutano
Wakati hilo likisubiriwa, zipo taarifa kuwa kuna
mvutano baina ya vyama ndani ya umoja huo hasa katika nafasi ya mgombea
urais baada ya kuwapo kwa watia nia zaidi ya mmoja.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya umoja huo
kilisema kuwa Kamati Kuu ya Ukawa ina kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa
maridhiano yanafikiwa ili kumpata mgombea atakayeungwa mkono na vyama
vyote katika jitihada za kuiondoa CCM madarakani.
“Licha ya kutangaza kugawana kata na majimbo yaliyobaki jina la
mgombea urais litatangazwa pia. Hilo litafanyika endapo mwafaka
utapatikana katika kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika kesho (leo).
Kikao kikiridhia chama gani kitoe mgombea, basi Watanzania watamjua hiyo
Jumamosi,” kilisema chanzo hicho.
Chadema na CUF bado viliendelea na vikao vyake vya
ndani jana. Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo
alisema hakuna taarifa ambayo ingeweza kutolewa jana.
Alipoulizwa juu ya makubaliano yaliyopitishwa
katika kikao cha Ukawa alijibu: “Hakuna maazimio yaliyofikiwa, bado tupo
katika mjadala.”
Kuhusu kuungwa mkono miongoni mwa vyama vingine
vya Ukawa kwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba aliyetangaza
nia, Mketo alisema hana taarifa.
Wenyeviti wenza wengine wa vyama hivyo
hawakupatikana kuzungumzia suala hilo. Hata walipopigiwa simu zao za
mkononi, ziliita pasi na kupokewa.
chanzo: MWANANCHI
chanzo: MWANANCHI
