Akitoa salamu zake kwa wagombea hao, Rais Kikwete aliwapongeza na kuwatakia mafanikio mema katika safari yao.
“Wale wanaogombea urais waliomo humu (bungeni)
nawatakia kila la kheri na nawashukuru kwa kuonyesha nia ya kunipokea
mzigo huu mzito. Nawatakiwa heri katika matamanio yenu,” alisema Rais
Kikwete ambaye aliingia Ikulu mwaka 2005.
“Mko wengi, wote ni vigogo na mmetupa kazi kama kamati kuwachuja kwa hiyo msitununie tukifanya maamuzi.”
Wakati akihitimisha hotuba hiyo, Rais aliwashukuru
watu mbalimbali waliofanya kazi kwenye Serikali yake, lakini hali
ilikuwa tofauti alipomtaja Lowassa ambaye alifanya naye kazi kwa miaka
miwili.
Alimshukuru pia, Makamu wake, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadaye wabunge na viongozi wengine.
Alianza kwa kuwashukuru huku akiwataja majina.
Kila alipotaja majina ya viongozi hao, wabunge walipiga makofi kwa
kugonga meza zao. Hata alipomtaja Dk Bilal na Pinda, wabunge hao
walishangilia kwa kawaida.
Hata hivyo, alipofikia kutaja jina la Lowassa,
kelele za wabunge zilikuwa maradufu, wengi wao wakipiga meza
kushangilia, hali iliyomfanya Rais Kikwete anyamaze kwa sekunde kama 50
na ndipo Lowassa aliposimama na kuinamisha kichwa kuonyesha kukubali
shukrani hizo.
Wabunge waliendelea kumshangilia hadi alipoketi na
ndipo Rais Kikwete akaendelea kutoa shukrani kabla ya kuhitimisha
hotuba yake ya saa mbili na dakika 20.
Awaweka wagombea gizani
Kuahirishwa kwa vikao vya juu vya uchujaji makada wanaowania
kugombea urais kwa tiketi ya CCM, kumesababisha wagombea, wapambe wao na
wanachama kubaki gizani kwa kutoelewa kinachoendelea na hivyo kutoa
nafasi ya kuenea uvumi na ubashiri wa aina mbalimbali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa awali na Katibu
wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye vikao vya juu vya uchujaji wa wagombea
vilikuwa vianze juzi, kwa Kamati ya Usalama na Maadili kujadili taarifa
za wagombea urais na kutoa ushauri kwa Kamati Kuu. Taarifa
zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa kikao hicho kilitarajiwa kuanza
usiku wa jana ingawa kulikuwa na utata mkubwa.
Ratiba hiyo ilionyesha kuwa kikao cha Kamati Kuu
kilikuwa kifanyike jana, lakini kutokana na sababu zisizojulikana
hakikufanyika na badala yake imeelezwa kitafanyika leo, siku ambayo
ilikuwa imepangwa rasmi kwa ajili ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) unaojumuisha wajumbe zaidi ya 400.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Mkutano Mkuu wa CCM
ambao ndiyo wenye jukumu la kutoa mgombea urais, ulipangwa kufanyika
kesho na keshokutwa, lakini taarifa zilizopatikana baadaye zilisema
utafanyika kwa siku moja tu ya kesho.
Nape alipotafutwa mara mbili kwa nyakati tofauti
jana, majibu yake yalikuwa mafupi; “ratiba niliyotoa ndiyo hiyohiyo,
ifuateni kama mnataka kuandika”.
Alipotafutwa jioni baada ya kuenea tetesi kwamba
vikao vyote vitafanyika leo, hakupokea simu lakini alituma ujumbe mfupi
wa maandishi ukisema: “Siwezi kuongea sasa… Samahani nipo kikaoni, tuma
meseji”. Lakini hata alivyotumiwa ujumbe hakujibu.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu walipoulizwa kikao
chao kingefanyika lini, walisema hawakuwa na taarifa na kwamba na wao
walikuwa wanasubiri kupewa taarifa.
Mmoja wa wajumbe wa NEC aliyekuwa akizunguka
kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, huku akionyesha amechoka, alisema:
“Hapa nilipo hata sifahamu tutafanya lini kikao, nipo tu nazunguka
hapa.”
Giza hilo ambalo limewakumba wagombea na wajumbe
wa vikao, pia limesababisha kuenea kwa tetesi dhidi ya hatima za
wagombea na kutoa fursa kwa wajumbe wenyewe kuzodoana.
“Mgombea wako keshamalizwa, kikao cha kamati ya
maadili kimeshamkata,” ni miongoni mwa tetesi walizokuwa wakirushana
roho wajumbe wa vikao vya CCM, ingawa taarifa za uhakika ni kuwa kikao
hicho kilikuwa hakijafanyika.
Wengine waliokuwa na uelewa mpana walijibu kwamba vikao havijafanyika, hivyo kuhoji mgombea angekatwa na kikao gani.
Taarifa nyingine zilidai kuwa Kamati ya Usalama na
Maadili ina dozi za baadhi ya wagombea maarufu na kwamba alama za
ufaulu kwenye kamati hiyo zimewamaliza wengi.
Wagombea wanena
Pamoja na ratiba ya vikao hivyo
kubadilikabadilika, makada waliojitokeza kuwania urais kwa tiketi ya CCM
hawakuonekana kusumbuliwa na jambo hilo.
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alisema hana
tatizo na kuchelewa kwa vikao hivyo kwa kuwa vina ratiba zake na
maandalizi yapo ndani ya ratiba. Alisema viongozi wataendelea kutoa
miongozo na anaamini msemaji wa chama ataendelea kuujulisha umma
kinachoendelea.
Mgombea mwingine, Dk Hamis Kigwangalla alisema
hakuwa na taarifa rasmi za kutofanyika kwa vikao kama vilivyopangwa,
lakini akasema hilo halikuwa na madhara kwa wagombea na anaona sababu za
kufanya hivyo ni kupunguza presha.
“Naamini vikao vyote vitakaa na chama chetu
kuvisogeza mbele ni jambo la kawaida tumeshazoea. Nikiwa mmoja wa
wagombea, sina shaka wala wasiwasi wowote, ratiba iliyopangwa ya vikao
hivi imekutana na jambo kubwa.
Rais anatakiwa kuvunja Bunge na baadhi ya wajumbe
watahudhuria shughuli hiyo, hivyo lazima visogezwe mbele,” alisema
mgombea mwingine January Makamba.
Mwalimu Banda Sonoko alisema kila kitu ni
maandalizi hivyo anaamini kesho watakuwa wamepata mgombea, kwani vikao
hivyo vimeingiliwa na mambo mengi, ndiyo maana vimesogezwa.
“Sina tatizo lolote, natambua mwenyekiti wangu pia
ni Rais ana shughuli nyingi. Hili ni jambo zito, wahusika wanahitaji
wasaa ili wasije kutupatia mgombea ambaye hafai, sidhuriki na hii
chelewa chelewa, nitavumilia na kujigharimia kwa muda wote lakini tupate
mgombea safi,” alisema Balozi Ali Karume.
Mjumbe wa kamati ya kampeni ya Lowassa, Hussein
Bashe alisema hili siyo jambo la ajabu, bali ni kawaida kutokana na
maelekezo ya chama vikao ni mpaka Julai 12.
“Kuahirisha vikao vya Kamati ya Maadili, Kamati Kuu na NEC siyo jambo la kutilia shaka,” alisema.
Msemaji wa Stephen Wasira, Masyaga Matinyi alisema
anaamini kanuni, taratibu na katiba ya chama vitaheshimiwa hivyo
mchakato utakuwa wa haki.
“(Wasira) Anaamini vikao vitafanyika kwa mujibu wa
taratibu zilizopangwa, hivyo kuahirishwa huko hakuwezi kuvuruga
mchakato,” alisema Matinyi.
Kada mwingine kwenye mbio hizo, Elidephonce Bilohe alisema
anamwomba Mungu ili kuahirishwa kwa vikao hivyo kumpe neema kwa jina
lake kupitishwa kuwa mgombea urais wa chama hicho.
“Jana (juzi) nilikwenda ofisi za CCM nikakutana na
ofisa wa ngazi ya juu ya chama akaniambia kama tukihitajika na kikao
chochote tutaitwa. Basi nikaondoka, nipo hapa nyumbani namwomba Mungu
anisaidie niweze kuipata nafasi hii,” alisema Bihole.
Boniface Ndengo alisema kuahirishwa kwa vikao hivyo vya mchujo wa wagombea anaona hakuna tatizo.
“Nilishafanya sehemu yangu niliyotakiwa, sioni kama kuna usumbufu wowote,” alisema Ndengo.
Leonce Mulende alisema suala hilo halimpi matatizo
ya kisaikolojia kwa sababu limewekewa programu za msingi, hivyo
anafikiri watafikia hatima vizuri.
Balozi Patrick Chokala alisema: “Wenye shughuli zao ndiyo wanajua sababu za kuchelewa, wacha tusubiri watamaliza tu.”
Imeandikwa na Midraj Ibrahim, Noor Shija, Sharon Sauwa (Dodoma) na Suzan Mwillo (Dar).