
Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akijiandikisha katika daftari la kudumu la
wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki(Biometric Voters
Register( BVR) katika kijiji cha Msoga, kata ya Msoga wilayani Bagamoyo
jana.Kulia akiangalia kwa makini ni mwandikishaji msaidizi Bi.Happyness
Thomas Misana na katikati ni Afisa TEHAMA kutoka ofisi yaTume ya Taifa
ya Uchaguzi Bi.Mariam Rajabu.Kushoto aliyesimama akishuhudia ni Mbunge
wa Chalinze Ridhwani Kikwete.

Afisa
TEHAMA kutoka ofisi ya Tume ya Uchaguzi Taifa Bwana Sanif Khalfan
akichukua alama za vidole vya Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wakati Rais
alipokwenda kujiandikisha kijijini kwake Msoga wilaya ya Bagamoyo.

Bwana
SANIF Khalfan ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka ofisi ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi akimpiga picha Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wakati Rais
alipokwenda kujiandikisha kupiga kura kwa kutumia teknolojia mpya ya BVR
kijijini Kwake Msoga.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitambulisho chake wakati wa zoezi la kujiandikisha kijijni kwake Msoga.

Mwenyekiti
wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva akimkabidhi Rais
Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kitambulisho chake cha kupiga kura baada ya
Rais Kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia
teknolojia ya BVR huko kijijini Msoga wilayani Bagamoyo.

Rais
Kikwete akimshukuru Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian
Lubuva baada ya kukabidhiwa kitambulisho chake cha kupiga kura baada
ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia
teknolojia ya BVR huko kijijini Msoga wilayani Bagamoyo. .
JUMLA ya watu milioni 11,248,194 wameandikishwa kwenye daftari la
kudumu la wapiga kura zoezi ambalo linaendelea kwa sasa hapa nchini
likiwa limeingia mkoani Pwani.
Hayo yalisemwa jana kwenye Kijiji cha Msoga kata ya Msoga wilayani
Bagamoyo na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa Damian Lubuva
alipokuwa anampa taarifa Rais Dk Jakaya Kikwete mara baada ya
kujiandikisha.
Bw. Lubuva alisema kuwa malengo ni kuandikisha watu milioni 21 hadi
23 kote nchini mara zoezi hilo litakapokamilika kati ya Julai mwishoni
au Agosti mwanzoni kama hakutatokea matatizo.
“Hadi sasa ni mikoa 11 inaendelea na zoezi ambayo ni Mwanza
Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro Morogoro na
jana ulianza mkoa wa Pwani,” alisema Lubuva.
Aidha alisema kuwa changamoto zilizojitokeza ni za kawaida hasa
kutokana na mfumo huu kuwa ni mpya kwani kila jambo jipya lina
changamoto zake.
“Mfumo huu ni mpya hivyo lazima kuwe na changamoto za hapa na pale
lakini zoezi linakwenda vizuri na tunaamini kuwa tutafanikiwa kama
tulivyopanga,” alisema Lubuva.
Mkoa wa Pwani una jumla ya vituo 1,752 na mashine za BVR 932 ambapo
kata ya Msoga kuna jumla ya vituo 17 zoezi hilo kwa mkoa wa Pwani
lilianza jana na litamalizika Julai 20.
chanzo: GPL