Jun 6, 2015

SAKATA LA FIFA, THABO MBEKI AHUSISHWA NA TUHUMA ZA RUSHWA

Rais wa zamani wa Afrika kusini, Thabo Mbeki.
Waziri wa Michezo wa Afrika Kusini, Fikile Mbalula, amesema rais wa zamani wa Afrika kusini, Thabo Mbeki, ndiye aliyeruhusu ulipwaji wa dola milioni 10 kwa FIFA, hela ambazo sasa zinadaiwa zilikuwa rushwa.
Serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikisisitiza kwamba fedha hizo zilikuwa ni sehemu ya mchango wa kusaidia kukuza soka katika nchi za Caribbean lakini waendesha mashtaka wa Marekani wanadai kitita hicho kilitolewa kama hongo kushawishi FIFA kutoa haki ya kuandaliwa mashindano ya kombe
la dunia ya 2010 katika nchi hiyo.
Mbeki mwenyewe hajatoa kauli yoyote kuhusiana na swala hilo. Barua inayosemekana iliandikwa na shirikisho la soka nchini Afrika kusini, inaonekana kuongeza uzito kwenye shutuma kwamba serikali ya nchi hiyo ilitoa malipo hayo kwa siri.
Madai ya ufisadi dhidi ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wamelitikisha shirikisho hilo na hata kupelekea rais wake, Sepp Blatter kujiuzulu ghafla ikiwa imepita wiki moja tu tangu achaguliwe tena kuongoza kwa miaka minne.
CHANZO: IRAN SWAHILI