Mwenyekiti chama cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akilakiwa na wanachama wa chama hicho alipokuwa akiwasili katika ukumbi wa mkutano kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia CUF Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi
(CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechukua fomu ya kugombea urais kupitia
chama hicho na kuahidi kupambana na rushwa huku akishangaa kuwapo
watuhumiwa wa ufisadi waliotakiwa kuwa mahabusu lakini wakichukua fomu
za kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.
Profesa Lipumba alisema iwapo atapatiwa ridhaa na
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupeperusha bendera ya umoja huo
atahakikisha anaunda Katiba yenye maoni ya wananchi na Serikali ya Umoja
wa Kitaifa ili kuwaunganisha Watanzania dhidi ya ufisadi.
Mwanasiasa huyo mkongwe katika upinzani aliwaambia
wafuasi wa CUF waliomsindikiza kuchukua fomu hiyo jijini hapa jana kuwa
ameamua kuwania kiti hicho kwa mara ya tano kwa kuwa kati ya viongozi
wa juu wa Ukawa anaamini ana sifa, uwezo, uadilifu, uwazi, uwajibikaji
wa kuwaunganisha Watanzania ili waondokane na rushwa na ufisadi
uliokithiri nchini.
Profesa Lipumba aliyekabidhiwa fomu hiyo na Katibu
wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu saa 6.55 mchana, alitaja
vipaumbele vyake kuwa ni kujenga misingi ya kuhakikisha watoto wanapata
fursa sawa ya maendeleo, ajira, afya, kulinda rasilimali za umma na
kupambana na ufisadi.
Profesa Lipumba aliyeanza hotuba yake ya takriban
dakika 45 kwa kutoa wasifu wa usomi na kazi mbalimbali za kiuchumi
alizozifanya kwa takriban miaka 40, alisema anafahamu bayana matatizo
mengi ya Watanzania kwa kuwa amezaliwa na kukulia kijijini.
Alisema matatizo hayo yamesababishwa na “siasa
mbovu za chama cha mapinduzi” ukiwamo ufisadi, hivyo iwapo atapatiwa
ridhaa ya kuwania kiti hicho cha juu, atakuwa na kazi kubwa ya kuleta
uongozi makini utakaohakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa
maendeleo ya watu wote.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais, hatakuwa na
msalie mtume na mafisadi na wote wanaohusika watawajibika kwa mujibu wa
sheria na taratibu.
“Inatisha sana kuona mafisadi wakubwa, wala rushwa
wakubwa badala ya kuwa ndani ya jela, wanachukua fomu za urais.
Tunahitaji kwa kufuata taratibu na haki, mafisadi hao watumikie vifungo
na mali zilirudishwe kwa umma walikofisadi,” alisema Profesa Lipumba
huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Iwapo atapatiwa nafasi ya urais, alisema katika
utawala wake atahakikisha watoto nchini wanapatiwa fursa sawa ya
maendeleo kwa kutoa huduma bora afya, lishe na elimu.
Alisema suala la ukuaji imara kwa watoto
halijapatiwa kipaumbele na kusababisha udumavu unaowanyima uwezo mkubwa
wa kufikiri pindi wanapokuwa wakubwa.
Kufumua Katiba inayopendezwa
Mwanasiasa huyo alisema anachukua fomu nchi ikiwa
njia panda baada ya Katiba Inayopendekezwa kuacha masuala ya msingi ya
uadilifu na uwajibikaji na kusababisha wachache kujinufaisha kwa rushwa.
Akielezea kwa kina juu ya Katiba Mpya, Profesa Lipumba alisema
Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya
Jaji Joseph Warioba iliweka misingi ya maadili ya nchi na kubainisha
kuwa chanzo kikubwa cha ufisadi ni zawadi ndogondogo lakini viliondolewa
na wanasiasa wasiopenda maadili.
“Mafisadi walihakikisha wanaving’oa vifungu vya
maadili na zawadi ili wakipatiwa zawadi waende kununua mboga. Tunahitaji
kazi kubwa kuyarudisha maoni yalitolewa na wananchi tuweze kuyalinda
kwa pamoja na kuyaheshimu ili uwazi, uwajibikaji na uadilifu ziwe ni
Tunu za Taifa.
“Uzuri wa katiba inayotokana na wananchi unaweza
kuitumia kuizaa Tanzania mpya kwa kuwaambia hii ni katiba yenu muilinde
na kuhakikisha viongozi wanawajibika,” alisema.
Serikali ya mseto
Alisema Ukawa ilianza bungeni kupigania maoni ya
wananchi kwa kujumuisha vikundi vingine vya kijamii hivyo akiwa rais
ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili iwaunganishe Watanzania
kupambana na ufisadi.
Profesa Lipumba pia alisema atapambana na tatizo
la ajira kwa kuhakikisha bandari zote nchini zinafanya kazi kwa ufanisi
ili kuzalisha kazi nyingi iwezekanavyo kukidhi mahitaji ya vijana.
Katika kuimarisha sekta ya afya, alisema
atahakikisha anapambana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kirahisi kama
malaria na kifua kikuu na kuwawezesha Watanzania kuwa na bima za afya.
Pia, alisema kutakuwa na mpango maalumu wa
kuwaenzi wazee ili waweze kuishi vizuri tofauti na sasa huku akibainisha
mipango yote hiyo inatekelezeka lakini sasa imeshindikana kutokana na
ufisadi wa kupindukia.
Profesa Lipumba alieleza dhamira yake ya kupitia
mikataba yote ya rasilimali nchini hasa iliyopo katika sekta ya madini
ili ziweze kuwanufaisha wananchi wote.
“Ili tufanikishe hayo ni lazima tuweke motisha kwa
wananchi kulinda rasilimali zao na ni lazima tuweke uwazi kwa viongozi
wa Serikali,” alisema.
Alisema iwapo Ukawa watakubaliana asimame mgombea
mwingine tofauti na yeye yupo radhi kumwachia na atahakikisha anampigia
kampeni kwa nguvu zote ili ashinde katika Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba.
chanzo MWANANCHI
Mtaalamu huyo wa uchumi pia alizungumzia maisha yake ya ndoa kwa
kueleza kuwa mke wake huwa hajihusishi na siasa kwa kuwa ni mfanyakazi
wa Shirika la Umoja wa Mataifa na taratibu zao haziwaruhusu kufanya
hivyo.
“Watu huwa wananiuliza nimeoa? Leo nawaambia
nimeoa na naruhusiwa kuwa nao hadi wanne, ila ninaye mmoja tu. Watu
wanapaswa kufahamu mimi ni mgombea wa urais siyo familia inagombea
urais… kuna watu wakipata uenyekiti wa chama, basi mke wake kapata
tiketi ya viti maalumu, sisi kwetu hayapo hayo, mtu apatiwe nafasi
kulingana na uwezo wake,” alisema Profesa Lipumba huku akikoleza kwa
salamu ya chama, “CCM kwishaa, kwishaa, kwisha kabisa, nyang’anyang’a,
ndembendembe, mlalo wa chali, kifo cha mende na akiitikiwa na wafuasi wa
chama hicho huku wakimshangilia.
Alisema akiingia madarakani anataka kuwa rais wa
kwanza wa Tanzania kupata Tuzo ya Mo Ibrahim kwa kutenda haki,
uwajibikaji na usawa kwa wananchi.
Maalim Seif
Awali, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad aliwauliza wafuasi wa chama hicho kuwa ni nani kati ya
waliotangaza nia kuwania urais kupitia CCM ambaye ni msafi.
Wafuasi wa chama hicho walimjibu kwa sauti ya pamoja, hakunaaa!
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
aliyetambulishwa juzi Pemba kuwania urais wa visiwa hivyo, alisema muda
wa mabadiliko ni sasa na Watanzania wamechoshwa na utawala kandamizi wa
CCM.
“Imebaki miezi mitatu, hakuna kulala tumechoshwa na utawala wa mafisadi unaokandamiza na kuonea watu,” alisema.
