.jpg)
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akifungua
pazia kuashiria ufunguza rasmi wa MASJID AQSAA katika kijiji cha Kiboja
Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja.
.jpg)
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akipena
mikono na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, baada ya
ugunguzi wa MASJID AQSAA na sala ya Ijumaa katika kijiji cha Kiboja
Mkwajuni.
.jpg)
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi
wa dini ya kiislamu nchini pamoja na waislamu mbali mbali wakisikiliza
hotuba ya Ijumaa iliyotolewa na Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh
Fadhil Soraha (hayupo pichani) katika msikiti mpya wa MASJID AQSAA
ulioko Kiboja Mkwajuni. Kushoto ni Kadhi Mkuu Sheikh Khamis Haji
akifuatiwa na Mufti Mkuu Sheikh Saleh Omar Kabi
.jpg)
Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, akitoa nasaha baada ya uzinduzi wa MASJID AQSAA Kiboje Mkwajuni.
.jpg)
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu walioshiriki katika ufunguzi wa MASJID AQSAA, Kiboje Mkwajuni.
.jpg)
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akiwahutubia waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria ufunguza wa
MASJID AQSAA katika kijiji cha Kiboja Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja.
Picha na Salmin Said, OMKR
Na Hassan Hamad (OMKR)
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
amewasisitiza waislamu nchini kuachana na tabia ya kugombania misikiti,
kwani haisaidii kuendeleza dini hiyo.
Amesema
misikiti ni nyumba za Mwenyezi Mungu, hivyo hakuna sababu kwa waislamu
kulumbana kwa sababu za kugombea uongozi au kutokana na tofauti ya
kimadhehebu.
Maalim
Seif ametoa nasaha hizo wakati akifungua msikiti wa Ijumaa MASJIDIL
AQSAA katika kijiji cha Kiboje Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja.
Amesema
Uislamu ni dini yenye nidhamu kamili, na kuwataka waumini wa dini hiyo
kufuata nidhamu hizo katika kuendesha mambo yao bila ya kukaribisha
malumbano na mifarakano baina yao.
Amewahimiza
waislamu wa eneo hilo kuuimarisha na kuuendeleza msikiti huo kwa
kuendeleza harakati za darsa, sambamba na kuwaandalia watoto muda wa
kutosha kuweza kuhudhuria katika darsa hizo ili kuwajenga kimaadili.
Amesema
madrasa zina mchango wa kipekee katika kuwaandaa watoto na kuwakuza
kuwa raia wema walioleleka katika maadili ya Kiislamu, na kwamba
waislamu bado wana jukumu la kuzianzisha madrasa kwa wingi na
kuhakikisha kuwa watoto wanapita katika darsa hizo kupata malezi
sahihi.
Amefahamisha
kuwa hivi sasa Zanzibar inahitaji malezi mazuri kwa watoto na vijana
kuliko wakati mwengine wowote, kutokana na matishio makubwa
yanayojitokeza na kuvurugika kwa maadili mema.
Amewakumbusha
waislamu kuchangia harakati za dini hiyo kwa kujenga na kuimarisha
misikiti na madrasa, kwani kila mmoja ana wajibu wa kutoa mchango wake
katika kuziendeleza nyumba hizo za Mwenyezi Mungu.
Aidha
Maalim Seif amewakumbusha waislamu kuendeleza umoja, maelewano, na
mshikamano miongoni mwao, na kujiepusha na chuki miongoni mwa waumini wa
dini hiyo na dini nyengine.
Amesema
serikali imefanya juhudi kubwa kuiwezesha jamii kuondokana na hasama,
chuki na kudharauliana na badala yake kujenga mazingira ya umoja,
mshikamano na maelewano, mambo ambayo yanapaswa kuungwa mkono kwa
vitendo.
Katika
hatua nyengine Maalim Seif ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa
waangalifu katika kuwachagulia vyuo vijana wao, ili kuepusha madhara
yanayoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa maadili .
Amesema
baadhi ya vyuo hasa vilivyoko nje ya nchi havina misingi mizuri ya
malezi, na kwamba bila ya kuwa waangalifu jamii inaweza kupoteza wengi
ambao hatimaye wanaweza kujitumbukiza katika vitendo viovu.
“Chagueni
vyuo vitakavyo wanufaisha vijana, sio kijana kwa sababu anakwenda
kusoma nje ya nchi umkubalie tu, wazazi na walezi ni lazima mufuatilie
kujua uhakika wa vyuo hivyo” alisisitiza.
Akizungumza
kabla ya hotuba ya Ijumaa, Sheikh Thabit Noman Jombo kutoka ofisi ya
Mufti wa Zanzibar amewahimiza waislamu wa eneo hilo kuutumia msikiti huo
kama sehemu ya kutolea taaluma.
Amesema
Zanzibar ilikuwa kitovu cha elimu katika nchi za Afrika Mashariki, na
hakuna budi kuienzi historia hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mapema
akisoma risala ya wazee wa msikiti huo Sheikh Abdalla Rajab,
amewashukuru waliojenga msikiti huo mkubwa katika kijiji chao, na
kuahidi kuutunza na kuweka darsa ambazo zitakuwa endelevu.
Amesema
uwepo wa msikiti huo ni faraja kwa wanakijiji na maeneo jirani, kwani
pia wameweza kuondokana na shida ya maji safi na salama iliyokuwa
ikiwakabili kwa kipindi kirefu.
picha habari kwa hisani ya michuzi media