“Masikio hayawezi kuvuka kichwa, kiongozi wa serikali usiyetaka
kuambiwa ukweli na chama nenda kalale, acha kazi.” Hii ni kauli ya
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye
aliyoitoa wakati akikemea ule aliouita uzembe wa Waziri wa Maliasili na
Utalii, Lazaro Nyalandu.
Nape na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana bado wanaendelea
kupaza sauti kuwa baadhi ya wateule wa mwenyekiti wao wa chama, Jakaya
Kikwete hawaendani na kasi ya kutumikia jamii.Mwaka jana waliibuka na
kibwagizo kuwa, serikali yao inayoongozwa na Rais Kikwete ina rundo la
mawaziri mizigo, utashi wao ukawa ni kumtaka mwenyekiti awatimue
wasikigharimu chama.
Wakati kionjo hicho cha mawaziri mizigo kikionekana kupoa, wameibua
kingine kinachoitwa waziri mzururaji; wakimaanisha Nyalandu. Wametoa
hoja ang’olewe akalale kwa kuwa ameonesha kuishindwa nafasi ya uwaziri.
Wamesema wazi kuwa, masikio hayazidi kichwa, tafsiri ni kwamba
wanaoingoza serikali ni masikio ya CCM ambacho ndiyo kichwa cha rais
hadi katibu tawala. Hapa ndipo ninapoitafakari CCM na serikali yake
kiasi cha kuchanganyikiwa.
Kwa nini? Nape na Kinana wanaposema karibu kila walikopita wamekutana
na migogoro ya ardhi ikiwahusisha wananchi, hifadhi za taifa na kwa
upande mwingine wawekezaji na waziri yupoyupo tu; anazurura, kuna kitu
cha kutafakari.
Najiuliza; Kinana anapomuona mzururaji Rais Kikwete aliyemchagua
katika nafasi hiyo ya uwaziri anakuwa wapi, kalala? Nape anapomuona
Nyalandu kuwa ameshindwa kutekeleza jukumu lake; Rais Kikwete, kasafiri?
Nachanganyikiwa kabisa!
Ukifuatilia ziara za Nape na Kinana zinazoitwa za kujenga chama kila
walipopita viongozi hao hotuba zao nyingi zimejaa ukosoaji kwa baadhi ya
watendaji wa serikali, kwa vinywa vyao wamekiri hadharani kuwa udhaifu
huo unakidhoofisha chama chao.
Jambo la kujiuliza; hivi kichwa (CCM) na masikio (watendaji) havina
ushirikiano ndiyo maana jamii inashuhudia mkanganyiko huo wa kimtazamo?
Ikiwa viungo hivi havishirikiani katika utendaji, wananchi
wanavigawanyaje ili kinachoonekana dhaifu wakichukie?
Tangu lini mchongoma ukazaa machungwa? Kamwe chemchemi ya maji
haiwezi kutoa maji matamu na maji machungu. Naomba nisikilizwe hoja
zangu kwa makini.CCM ya Nape na Kinana, mwenyekiti wake ni Rais Kikwete
ambaye ni mkuu wa uteuzi wa karibu nafasi zote nyeti za nchi hii, nafasi
hizohizo ndizo zinazopigiwa kelele na wasafisha chama kuwa ni dhaifu
ki-utendaji!
Kwa nini tusifike mbali zaidi ya fikra hizo, tuvuke mipaka ya ufahamu
mpaka tuusogelee ukweli kuwa anayewaangusha siyo Nyalandu na uzururaji
wake bali aliyemteua ambaye ni mwenyekiti wa CCM.
Nashangaa
kuaminishwa kuwa chama kinaweza kuwa mtetezi wa wanyonge kwa kiwango
wanachoonesha akina Kinana, kuipita serikali ambayo inaongozwa na
mwenyekiti wa Kinana.
Hivi mashauriano ya chama kifanye nini hawa akina Nape wanayafanyia
nyumbani kwao au ofisini? Wanajipangia watakavyo au vikao vya chama na
ridhaa ya viongozi wa ngazi za juu akiwemo mwenyeti ndiyo vinavyotoa
baraka ya ziara na kupokea mrejesho wa kilichofanywa na watumwaji!
Ikiwa chama kinaongozwa kwa mfumo, iweje rais ambaye ni mwenyekiti
asijue kuwa, Nyalandu ni mzururaji na kumtimua kazi mara moja! Waliitwa
mawaziri mizigo wakaendelea kudunda kwenye nafasi zao; Nyalandu kaambiwa
aache kazi lakini bado anapanda ndege na kulipwa mshahara unaotokana na
kodi za wananchi.
Naomba Nape awaambie wananchi wafanye nini ili watenganishe kichwa na
masikio kwa sababu wamechoshwa na umaskini. Asipofanya hivyo ipo siku
wataamua kukata shingo, wakiondoe kichwa pamoja na masikio yake kisha
wavitupe jalalani! Nachochea tu.
kwa hisani ya GPL